Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WIZARA ya Uwezeshaji Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto ya
Zanzibar, imesema imeanza kuufuatilia mtandao uliokuwa ukiwahusisha
vijana wenye umri wa miaka 16 na kuendelea, kufanya mapenzi ya jinsi
moja Unguja na Pemba.
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Msham Abdalla Khamis alisema hayo
alipozungumza na waandishi wa habari, akieleza hali ya matukio ya
vitendo vya udhalilishaji wa jinsi. Pia, alikuwa akieleza juhudi
zinazochukuliwa na Serikali kupambana na matukio ya aina hiyo ambayo
yamekuwa tishio kwa maendeleo ya jamii visiwani humu.
Alisema kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na taasisi mbalimbali,
ikiwemo za dini ya Kiislamu imebaini kuwepo kwa kundi la vijana
wanaofanya mapenzi ya jinsi moja na kwamba hali ni mbaya zaidi katika
kisiwa cha Pemba.
Khamis alisema, kitendo cha vijana kuanzia umri wa miaka 16
kujishughulisha na vitendo vya ngono ya jinsi moja ni kinyume na maadili
ya taifa la Tanzania na hatari kwa vijana ambao ni tegemeo na nguvu
kazi ya taifa kukosa nguvu za kazi, kwani watakuwa wameathirika na hali
hiyo.
“Zipo taarifa tunazifanyia kazi kwa sasa ambazo ni kuongezeka kwa
vitendo vya mapenzi ya jinsi moja kwa wanaume kwa wanaume kuanzia umri
wa miaka 16 Unguja na Pemba. Madhara yake makubwa ni kuwa na vijana
wasio na tija kwa taifa hapo baadaye,” alisema.
Alisema, matukio hayo yanachangiwa na kuporomoka kwa maadili ikiwemo
vijana wengi hivi sasa kuiga utamaduni wa kigeni, kudanganywa kwa tamaa
zilizopindukia ya anasa. Ofisa katika Wizara ya Uwezeshaji Ustawi wa
Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, Halima Masheko alithibitisha kuwepo
kwa taarifa hizo ambazo wizara imeanza kuchukuwa juhudi za kuutafuta
mtandao unaojishughulisha na kuwaingiza vijana katika mapenzi ya jinsi
moja.
Naye ofisa katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali huko Pemba,
aliyekataa kutaja jina gazetini, alikiri kuwepo kwa wimbi la vijana wa
kiume kujiingiza katika vitendo hivyo. Alisema, katika shule moja
visiwani Pemba (hakuitaja), wanafunzi walidiriki kutaka wapenzi hao wa
jinsi moja kutengewa darasa lao maalumu kutokana na kuonesha hadharani
mahusiano yao na kuwakera wenzao.
Utafiti wa Tume ya Ukimwi ya Zanzibar (ZAC) umebaini kwamba kundi
linalofanya mapenzi ya jinsi moja la wanaume kwa wanaume linaongoza kwa
maambukizi ya ugonjwa huo Zanzibar kwa asilimia 12.
CHANZO; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment