Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.
Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza uamuzi wake wa
kutoshiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar, uliopangwa kufanyika Machi
20, mwaka huu, na kutoa sababu zilizokifanya kufikia uamuzi huo.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salum
Jecha, alitangaza msimamo wa tume hiyo kuwa ni kurudia uchaguzi huo
baada ya kubaini kuwapo kwa dosari katika uchaguzi uliofanyika Oktoba
25, mwaka jana.
Tamko hilo, lilitolewa jana na Mwenyekiti wa CUF, Dk. Twaha
Tasilima, huku akisema sababu zilizowafanya kutoshiriki ni kwamba
uchaguzi huo si halali kwa kuwa uchaguzi halali ulishafanyika Oktoba,
25, mwaka jana.
Alisema sababu nyingine kubwa ni kutokana na matamko yote mawili
ya Mwenyekiti wa ZEC, kutokuwa halali na kwenda kinyume cha Katiba ya
Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na. 11 ya 1984.
“Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya
Uchaguzi ya Zanzibar, kinachotoa uwezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar na hata kwa tume yenyewe kufuta uchaguzi au
kuitisha uchaguzi wa marudio,” alisema Tasilima.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, sababu nyingine ni kwamba upande wa
uchaguzi wa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani ulikamilika na
washindi wote kupewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua kuwa
washindi halali.
“Kwa upande wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, alisema matokeo
yalishabandikwa nje ya vituo vya majumuisho vya majimbo yote 54 na
kwamba kilichokuwa kinaendelea baada ya hapo ni kuhakiki matokeo kutoka
majimboni na kazi hiyo ilishakamilika kwa majimbo 40 na majimbo 31
yalishatangazwa kabla ya Jecha kutangaza kufuta uchaguzi huo,” alisema.
Alisema pia Baraza Kuu la Uongozi la CUF lilifikia uamuzi wa
kususia uchaguzi huo kutokana na kutiwa moyo na taasisi na jumuiya zote
za kimataifa na kikanda zikiwamo Jumuiya ya Madola, Umoja wa Ulaya (EU),
Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika
(SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Pia alisema Marekani na Uingereza zimeonyesha msimamo wao wa
kuungana na Wazanzibari na kutetea haki yao ya kidemokrasia na uamuzi
halali uliofanya katika uchaguzi mkuu, uliomalizika mwaka jana.
WITO KWA WAZANZIBAR
Kikao hicho cha baraza kilichofanyika jana katika ofisi za Makao
Makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam kwa saa nne, kiliazimia kuwa
Wazanzibari wote wanaoipenda nchi yao na ambao wanaamini katika utawala
wa sheria, demokrasia na kuheshimu Katiba na sheria za nchi kutoshiriki
uchaguzi huo wa marudio.
Dk. Taslima alisema Wazanzibari wanapaswa kudai haki yao ya msingi ya uamuzi wa kupiga kura Oktoba 25, mwaka jana kwa amani.
Baraza hilo lililokuwa na ajenda moja pia lilijadili na kutolea
uamuzi kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,
kuandika barua ya kutaka vyama vya siasa kushiriki uchaguzi wa marudio.
“Baraza Kuu halikutarajia kama Jaji Mutungi angefanya kazi ya
kutumikia maslahi ya watawala na kushindwa kukemea uovu wa kubaka
demokrasia na haki za watu,” alisema.
Alisema pia wamesikitishwa na kitendo cha Rais Dk. John Magufuli,
kukwepa dhamana na wajibu wake kama Mkuu wa Nchi, kuiacha njiani kazi
aliyoianza ya kutafuta ufumbuzi wa uchaguzi huo.
“Baraza linamtaka Rais Magufuli kujitathmini na kujiuliza anajiweka
vipi na kutoa taswira gani mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya
kimataifa kutokana na kutosimamia ahadi yake aliyoitoa mbele ya
Watanzania wakati akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya kazi na vyama
vya CUF na CCM ili kutafuta ufumbuzi wa jambo hili,” alisema.
Pia alisema CUF inalaani matumizi ya nguvu kubwa ya vyombo vya
ulinzi na usalama dhidi ya wananchi wasio na hatia na ambao wamekuwa
watulivu, licha ya vitendo vingi vya uchokozi wa makusudi na hata
mashambulizi ya hujuma dhidi yao yanayofanywa na makundi ya vijana wa
CCM waliowekwa katika kambi kadhaa kisiwani Unguja.
Sambamba na hilo, waliiomba jumuiya ya kimataifa hasa taasisi
zinazosimamia haki za binadamu na zinazopambana na makosa ya jinai
kimataifa, ikiwamo Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC)
kufanya uchunguzi wa kauli na matendo ya uhalifu, uvunjwaji mkubwa wa
haki za binadamu na ubaguzi.
KAULI YA MAALIM SEIF
Akijibu maswali mbalimbali kutoka kwa waandishi wa habari jana,
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema kususia uchaguzi
huo kuna heri kuliko kufanya uchaguzi ambao wana uhakika CCM imejipanga
kushinda.
Alisema CCM imejipanga kutumia vyombo vya dola kuhakikisha inapata
ushindi, hivyo CUF kushiriki uchaguzi huo ni sawa na kujitia kitanzi na
kuchinjwa shingo.
“Hatuwezi kurudia uchaguzi usiyo halali na kama kususia uchaguzi ni
kuwapa uhalali wa kutawala hata tusiposhiriki ni lazima CCM kitashinda
kwani tayari kiongozi mmoja alishatangaza kuwa baada ya upigaji kura
kumalizika saa 10:00 jioni watatangaza matokeo yao saa 2:00, hii ina
maana kuwa tayari wana mshindi na sisi tunaenda kushiriki haramu,”
alisema.
Alisema pia kwa vyama vingine kushiriki uchaguzi huo, hakuwezi
kuzuia azma ya serikali kumtangaza Dk. Ali Mohammed Shein wa CCM kuwa
mshindi kwa kuwa vyama hivyo havina nguvu na kwamba hakuna chama
kinaweza kupata zaidi ya kura 400.
SMZ YAWEKA MSIMAMO
Wakati CUF ikitangaza uamuzi huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ) inasema uchaguzi wa marudio uko pale pale kama ulivyopangwa.
Kadhalika, uamuzi wa Chama cha CUF kususia uchaguzi wa marudio umewagawa wanasiasa na wanaharakati visiwani Zanzibar.
Mgawanyiko huo umetokana na kuwepo wanaounga mkono msimamo wa CUF
wa kususia uchaguzi wa marudio na wanaopiga azimio la Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa kugomea uchaguzi uliyopagwa kufanyika Machi 20, mwaka
huu.
Akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana, Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, alisema uchaguzi wa marudio
utafanyika kama ulivyopangwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar na kwamba
serikali inaendelea kukamilisha gharama za kufanikisha uchaguzi huo.
“Kama wao wamejitoa sawa lakini uchaguzi utafanyika kama
ulivyopangwa kwa sababu suala la kushiriki uchaguzi au kutoshiriki ni la
hiari kwa chama,” alisema.
Balozi Seif alisema ZEC ilifuta matokeo ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba
25, mwaka jana, baada ya kujiridhisha kuwa ulipoteza sifa na viwango
vya kuwa uchaguzi huru na wa haki.
Kwa upande wake, mwanasheria mkongwe wa Zanzibar, Awadhi Ali Said,
alisema uamuzi wa CUF ni sahihi katika kulinda Katiba na misingi ya
utawala bora.
Alisema kuwa uamuzi wa kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu yalikuwa
batili na kitendo cha kuingia katika uchaguzi sawa na kuhalalisha
ubatili wake.
Awadhi alisema Jecha alifuta matokeo ya uchaguzi kibabe bila
kuzingatia matakwa ya Katibva na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar na
kwamba kitendo hicho kimeiingiza nchi katika sokomoko la kisiasa na
mgogoro wa kikatiba. Alishauri hekima na busara kutumika badala ya
kulazimisha kufanyika kwa uchaguzi huo.
Pia alisema kukosekana mpatanishi baada ya kufanyika kwa mazungumzo
ya kutafuta muafaka wa mgogoro wa uchaguzi, ndilo chimbuko la kukwama
mazungumzo hayo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Tadea, Juma Ali Katibu,
ambaye alikuwa mgombea urais wa Zanzibar, alisema kama juhudi za
kutafuta muafaka zimekwama, CCM na CUF wakaribishe wapatanishi kutoka
nje.
Alisema Zanzibar inapita katika mazingira magumu ya kisiasa kwa
kufanyika uchaguzi wa marudio kabla ya kupatikana kwa maridhiano baina
ya pande mbili zinazovutana.
MSIMAMO WA CCM
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema chama
chake kimefunga mjadala wa malumbano ya uchaguzi na badala yake
kinajitayarisha na uchaguzi wa marudio.
Alisema kuwa hatima ya Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar (SUK)
itajulikana baada ya kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa marudio na kuwataka
watu kuacha kutabiri kifo cha serikali hiyo baada ya washirika pamoja
kugoma kushiriki.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa si ya CCM na CUF. Chama chochote
kinaweza kuingia na kuunda serikali ya pamoja kama kitakidhi mashariti
ya Katiba ya Zanzibar,” alisema Vuai.
Kuhusu CUF kususia uchaguzi huo, alisema hakuna madhara yoyote
kutokana na vyama 14 ambavyo vilijitokeza katika uchaguzi wa awali
kukubali kushiriki.
Kuhusu kushiriki uchaguzi huo, Vuai alisema CCM imeamua kuingia
katika uchaguzi wa marudio baada ya kujiridhisha kuwa uchaguzi wa Oktoba
25, mwaka jana, ulivurugwa na wasimamizi wa uchaguzi na si viongozi wa
tume hiyo.
Alisema wasimamizi wa uchaguzi wa vituo, majimbo na wilaya ndiyo
walivuruga uchaguzi mkuu na serikali inapaswa kuchukua hatua za
kisheria.
Msimamo huo wa CCM unashabihiana na wa serikali uliotolewa jana
Bungeni kwamba suala hilo limemalizika kwa kuwa tume imeshatangaza kuwa
utarudiwa na tarehe ya kufanya hivyo imeshapangwa.
Katika msimamo wake huo, serikali ilitangaza kuwa mjadala huo
umeshafungwa na kwamba hauwezi kujadiliwa tena ndani ya Bunge, hasa
katika kipindi hiki ambacho wabunge wanajadili hotuba ya Rais Dk. John
Magufuli.
Huku CCM na serikali zikitoa msimamo huo, mwanasiasa mkongwe Hassan
Nassor Moyo, alisema uamuzi uliofanywa na CUF ni mzito, hivyo
anahitaji muda kuangalia mwelekeo wa upepo wa kisiasa wa Zanzibar.
“Suala hili gumu kidogo. Niache niangalie upepo wa siasa
unavyokwenda kabla kulitolea maoni yake,” alisema Moyo ambaye ni Waziri
wa kwanza Katiba ya Sheria baada ya kuasisiwa kwa Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar mwaka 1964.
Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, alipoulizwa, alisema yeye si
msemaji wa Tume na kutaka atafutwe Jecha ambaye hakupatikana baada ya
simu yake kuita mara kadhaa bila kupokewa au kujibu maswali kupitia
ujumbe mfupi wa simu (sms).
Uamuzi wa CUF kujitoa katika uchaguzi umeibua mjadala mkali katika
Manispaa ya Mji wa Zanzibar huku wafuasi wa CCM wakionekana katika
mazingira ya furaha na wafuasi wa CUF wakijadili kwa umakini uamuzi wa
Baraza kuu la Uongozi.
Imeandaliwa na Mary Geofrey, Dar na Mwinyi sadallah, Zanzibar
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment