Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Zanzibar. Makada wa CUF, ambao waligombea uwakilishi na udiwani na kutangazwa kuwa washindi kabla ya matokeo kufutwa, wamewasilisha barua kwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kupinga hatua zozote za kurudia kupiga kura.
Hatua ya makada hao imechukuliwa na wagombea wote 27 waliotangazwa washindi wa viti vya uwakilishi sambamba na magombea 37 waliotangazwa washindi wa udiwani katika majimbo yote 18 ya Pemba na kupewa vyeti vya ushindi kabla ya uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka jana kufutwa na Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha.
Uchaguzi wa marudio umepangwa kufanyika Machi 20 baada ya Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi wa rais, wawakilishi na wadiwani yaliyotokana na uchaguzi huo, akidai sheria na kanuni zilikiukwa.
Habari zinasema kuwa barua za makada hao ziliwasilishwa ofisi za uchaguzi za wilaya zote nne za Pemba, kuanzia Februari Mosi mpaka jana. Akizungumza na gazeti hili kwa niaba ya ‘wawakilishi’ hao, Said Ali Mbarouk aliyepewa cheti cha ushindi wa Jimbo la Gando, Mkoa wa Kaskazini Pemba, alisema wamechukua hatua hiyo kwa kuwa taratibu zote halali za Uchaguzi Mkuu zilikamilika kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi Nambari 11 ya Mwaka 1984. Alisema wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo walimtangaza yeye na wenzake kuwa washindi wa nafasi hizo majimboni baada ya kupata kura nyingi.
Alisema sambamba na kutangazwa huko, watendaji hao wa ZEC waliwakabidhi shahada rasmi za ushindi na hivyo kutambulika kuwa wawakilishi wateule pamoja na madiwani halali wa majimbo na wadi husika kwa mujibu wa sheria.
“Mtakumbuka kuwa katika uchaguzi huo hakuna malalamiko yoyote yaliyowasilishwa na mhusika yeyote kwa mujibu wa sheria, hivyo washiriki na wadau wote, wakiwamo ZEC, tuliridhia kuwa uchaguzi ulikwenda kwa mujibu wa sheria na ulikuwa huru na haki, jambo ambalo pia lilithibitishwa na waangalizi huru wa ndani na nje ya nchi na pia ZEC,” alisema Mbarouk.
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI.
CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment