Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ametoa changamoto kwa
watendaji wa mahakama za watoto nchini kuongeza kasi, ari na kubuni
mbinu bora zaidi zitakazowezesha mahakama hizo kumaliza kesi zao haraka.
Katika hotuba yake baada ya kuweka jiwe la msingi la jengo la
Mahakama ya Watoto Mahonda katika Mkoa wa Kaskazini Unguja juzi, Dk
Shein alisema pale ambapo ushahidi wa kesi hizo upo, hakuna sababu za
mahakama kuchelewesha kesi hizo.
Hata hivyo alikiri kuwa uendeshaji wa kesi za udhalilishaji watoto
umekuwa ukikumbana na mazingira magumu hasa pale watu wanaopaswa kutoa
ushahidi mahakamani wanapokataa kufanya hivyo.
“Naamini mahakimu hawana nia ya kuchelewesha kesi hizo, lakini ukweli
ni kuwa kesi hizo zina mambo mengi magumu ikiwemo mashahidi kukataa
kufika mahakamani kutoa ushahidi,” alisema Dk Shein.
Alifafanua kuwa ni kweli ucheleweshaji kesi za udhalilishaji watoto
na wanawake unasababisha manung’uniko kutoka kwa wananchi na taasisi
zinazofuatilia kesi hizo, lakini aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali
itaendeleza jitihada zake kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa kwa
mujibu Sheria ya Mtoto ya Zanzibar, Namba 6 ya mwaka 2011 pamoja na
mikataba mingine ya kimataifa kuhusu haki za watoto.
Alibainisha kuwa ujenzi wa mahakama hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa
Mkakati wa Miaka Mitano (2013- 2018) wa Mapitio na Marekebisho ya Sheria
ya Watoto ambao umelenga kulinda haki za watoto wenye matatizo ya
kisheria.
Aliipongeza Idara ya Mahakama kwa kushirikiana na taasisi nyingine
zinazoshughulikia kesi za udhalilishaji watoto kwa kuchukua hatua
mbalimbali za kuhakikisha kuwa kesi hizo zinashughulikiwa haraka na
kutolewa hukumu.
Katika maelezo yake kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Jaji Mkuu wa
Zanzibar, Omar Othman Makungu alieleza kuwa ujenzi wa mahakama hiyo
kunafanya idadi za mahakama za watoto kufikia tatu; ya Vuga katika Mkoa
wa Mjini Magharibi na Chake Chake ambayo itakuwemo katika Jengo la
Mahakama mjini Chake Chake, Kusini Pemba.
Alisema ujenzi wa mahakama hiyo ambao umefadhiliwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa gharama ya Sh milioni
77, unatarajiwa kukamilika mwezi ujao.
CHANZO: HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment