Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
AKIZUNGUMZA kwa mara ya kwanza tangu atoke mahabusu, Katibu wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Shehe Ponda Issa Ponda
amemuomba Rais John Magufuli kutimiza ahadi yake ya kushughulikia hali
ya kisiasa visiwani Zanzibar.
Ponda amemtaka Rais Magufuli kutekeleza ahadi yake aliyoitoa bungeni
juu ya kufuatilia hatma ya hali ya kisiasa visiwani Zanzibar na kutoa
tamko la yale yaliyofikiwa katika mazungumzo ya kutafuta suluhu
yaliyokuwa yakihusisha pande mbili zinazovutana za Chama cha Wananchi
(CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Rais achukue ahadi yake aliyoitoa bungeni, ana wajibu wa kuitekeleza
kwa vitendo na ahakikishe mzozo huu anaupatia ufunbuzi bila ya
kuitumbukiza Zanzibar kwenye dhiki na uhasama,” alisema Ponda.
Pia alisema vyombo vya usalama vilivyopo Zanzibar vipo kwa amri yake
hivyo endapo patatokea jambo lolote kabla ya kumaliza mzozo wa kisiasa
uliopo visiwani humo ni yeye atakayelaumiwa.
Ponda alisema wao kama Jumuiya na Taasisi za Kiislamu wanaunga mkono
hatua za mwanzo zilizochukuliwa kunusuru hali ya kisiasa Zanzibar kwa
kufanya mazungumzo baina ya vyama hasimu vya CUF na CCM pamoja na kuunga
mkono ahadi ya Rais Magufuli ya kushughulikia mzozo huo aliyoitoa
wakati akizindua Bunge.
Aidha, amehoji ukimya uliopo hadi sasa kwani Watanzania hawajapewa
taarifa ya pamoja kutoka CCM na CUF kuhusu mazungumzo waliyofanya
yameishia wapi na yapi wamekubaliana na yapi hawajakubaliana na nini
hatima ya mazungumzo yao.
Shehe Ponda aliyekuwa pamoja na msemaji wa Shura ya Maimamu Tanzania,
Shehe Rajabu Katimba, alikanusha taarifa iliyotolewa jana kuwa Kiongozi
wa Uamsho, Shehe Farid Ahmad ameunga mkono uchaguzi huo wa marudio.
“Tumemtembelea Shehe Farid gerezani, lakini pia tulikutana na
wanasheria wake pamoja na viongozi wa gereza kutaka kujua kama aliandika
barua yoyote na si yeye wala mwanasheria au magereza waliothibitisha
kufanya hivyo naye kutuomba kukanusha taarifa hizo na kusema hazina
ukweli wowote,” alisema Shehe Ponda.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment