Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania,
Sheikh Ponda Issa Ponda, ameibuka kupinga kurudiwa kwa uchaguzi wa
Zanzibar na kumkumbusha Rais Dk. John Magufuli, atimize kwa vitendo
ahadi aliyoitoa bungeni ili kunusuru visiwa hivyo kutumbukia kwenye
uhasama.
Msimamo wa taasisi hiyo umetolewa siku moja baada ya Baraza la
Waislamu Tanzania (Bakwata) mkoa wa Dar es Salaam, kutoa tamko la kuunga
mkono kurudiwa kwa uchaguzi huo mwezi ujao.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, juzi alisema
kurudiwa kwa uchaguzi huo ndio njia pekee ya kumaliza mgogoro wa kisiasa
visiwani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Sheikh Ponda alisema uchaguzi uliofanyika mwaka jana kwa pande zote za
Muungano uliosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC), ulikuwa mzuri, huru na haki kwa mujibu wa
ripoti za waangalizi.
Alisema Rais wa Muungano, wabunge na madiwani walipatikana kwa
uchaguzi huo na sehemu ya Zanzibar wabunge wa Bunge la Muungano,
walipatikana katika uchaguzi uliosimamiwa na ZEC na matokeo yake
wanayaheshimu.
“Kwa sababu ambazo hazina msingi wowote, mwenyekiti wa ZEC alifuta
uchaguzi wote wa kuwapata viongozi wa Zanzibar, hatua ile haikuwa halali
kwa sababu mbili Kuu, moja ni Tume baada ya kutoa matokeo haina
mamlaka kisheria kufuta matokeo,” alisema na kuongeza:
“Uamuzi wa kufuta matokeo hata kama Tume ingekuwa na mamlaka,
maamuzi yale hayakuwa ya tume bali ni maamuzi ya mtu mmoja,” alisema.
Sheikh Ponda alisema kwa sababu hizo uchaguzi wa Zanzibar na
matokeo yake, bado ni halali na kuurudia ni kosa na ni kupanda mbegu
mpya ya chuki miongoni mwa wananchi.
Aliongeza kuwa wanaunga mkono hatua za mwanzo zilizochukuliwa
kunusuru hali ya kisiasa, kwa kufanya mazungumzo baina ya vyama hasimu
vya CUF na CCM.
Kadhalika alisema wanaunga mkono ahadi ya Rais Magufuli, aliyoitoa
bungeni ya kushughulikia mzozo huo kwa kushirikiana na mgombea wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad , na Rais Dk. Shein kupata suluhu.
“Mpaka sasa Watanzania hatujaambiwa kwa taarifa ya pamoja kutoka
CCM na CUF, mazungumzo waliyofanya yameishia wapi yepi wamekubaliana na
yepi hawajakubaliana na nini hatma ya mazungumzo yao,” alisema.
“Tunapinga vikali uamuzi wa ZEC kutangaza tarehe ya kurudia
uchaguzi kabla ya ufumbuzi wa mambo ya msingi na ya kisheria kupatikana,
hatua hiyo inaweza kuleta fujo hasama na kuharibu utangamano
uliopatikana kwa kipindi cha miaka ya karibuni Zanzibar,” alisema.
Alisema ushauri wa Jumuiya kwa Rais Magufuli ni kutekeleza kwa
vitendo ahadi yake ili kuhakikisha mzozo huo unapatiwa ufumbuzi bila
kuitumbukiza Zanzibar kwenye uhasama.
SOURCE:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment