Home » » Waziri avunja mkataba wa mwekezaji na kijiji

Waziri avunja mkataba wa mwekezaji na kijiji

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene amevunja mkataba baina ya mwekezaji wa kigeni na kijiji cha Chole wilayani Mafia.
Amechukua uamuzi huo kutokana na kijiji kutokuwa na haki ya kumiliki Mali Kale, ambazo kisheria zote humilikiwa na Serikali Kuu.
Mkataba uliovunjwa na Simbachawene ulikuwa ukihusu Kampuni ya Chole Mjini Conservation and Development Company Ltd, inayomilikiwa na Jean Devillies na mkewe, Ann Devillies na kijiji cha Chole.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chole kilichopo katika kata ya Jibondo wilayani Mafia, Simbachawene alisema eneo la Mali Kale ambalo zamani lilikaliwa na Waarabu na baadaye Wajerumani ni mali ya Serikali Kuu na kwamba kijiji hakikuwa na nguvu ya kisheria ya kumiliki eneo hilo.
Simbachawene aliongeza kuwa mara baada ya nchi kupata Uhuru, mali kale zote zilichukuliwa na Serikali Kuu na kwamba kijiji bila kushirikisha serikali kilikosa nguvu ya kisheria kumiliki eneo hilo.
“Mkataba huu ambao mwekezaji anaona ni mkataba sahihi kwake na unamfanya kuhisi kuwa ana haki zote, unaonekana una tatizo kwa sababu umeingiwa mwaka 2007 lakini kabla ya mwaka 2007 mwekezaji huyu alikuwa na hati,” alisema.
Waziri huyo alisema kipengele cha 227 kinaeleza kuiwezesha kampuni kupata hati miliki ya eneo kutoka kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya eneo lote, ambalo kwa wakati huo lilikuwa tayari linamilikiwa na kampuni hiyo.
Simbachawene alifafanua kuwa kipengele hicho, kina matatizo kwani maana yake ni kuwa kijiji kinatakiwa kiiwezeshe kampuni kupata hati wakati Mkataba huo unaandaliwa tayari kampuni hiyo ilikuwa na hati. Kipengele kingine kilichokuwa na utata, kwa mujibu wa mkataba huo ni kile cha 228 ambacho kinasema kutoruhusu mtu yeyote au kampuni au taasisi yoyote bila makubaliano na kampuni isipokuwa kwa mkazi wa Chole.
Waziri Simbachawene alisema kuwa kipengele hicho, kinakiuka sheria za nchi kwa kuzuia wawekezaji wengine kufanya biashara ya utalii katika kijiji hicho. Hivyo, Waziri alisema kuwa kijiji hakikuwa na mamlaka ya kuingia Mkataba na mwekezaji kwa ajili ya eneo la Mali Kale na hivyo Mkataba huo ni batili na hauwezi kutambulika kisheria kama mwekezaji huyo anavyoamini.
Waziri Simbachawene alisema kuwa Mkataba huo hauna nguvu ya kisheria na hivyo haupo, na kwamba mwekezaji huyo kwa sasa hana mamlaka ya kumiliki eneo hilo ambalo ni mali ya Serikali Kuu.
HABARI LEO 

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Tone multimedia company Limited
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa