Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka Wawakilishi, Wabunge na Madiwani wa
Chama hicho kujenga utamaduni wa kutoa taarifa za utekelezaji wa Ilani
ya CCM ya mwaka 2015/2020 kila baada ya miezi mitatu ili kuongeza
ufanisi wa kiutendaji.
Rai
hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho Zanzibar, Vuai Ali
Vuai alipokuwa akizungumza na Kamati ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
wanaotokana na CCM Zanzibar huko Afisini Kwake Kisiwandui Mjini hapa.
Alisema
viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi mbali mbali za kimaendeleo ambazo
ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya CCM, lakini zimekuwa
hazijulikani kwa baadhi ya wananchi na viongozi wa Chama kutokana na
kutofuatwa utaratibu wa kutoa taarifa rasmi kila baada ya miezi mitatu
ili zijadiliwe na ngazi husika kama ibara ya 189 ya ilani ya CCM
inavyoelekeza.
Vuai
aliwakumbusha Viongozi hao kwamba licha ya majukumu waliokuwa nayo
katika vyombo vya kutunga sheria bado wana jukumu kubwa la kuhakikisha
wanawatumikia wananchi kwa ufanisi katika kupunguza kero na changamoto
zinazowakabili katika maeneo yao.
“Nakukumbusheni
kwamba suala la kutoa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika
majimbo yenu ni muhimu sana kwani ndio kipimo cha utendaji wenu kwa
wananchi, na hatua hiyo itatoa fursa kwa viongozi mbali mbali wa chama
kuhoji ni kwa namna gani kila kila kiongozi anatekeleza wajibu wake kwa
wananchi na chama kwa ujumla.”
Kwani
hata kwa upande wa Chama Makao Makuu tunatoa taarifa mbali mbali za
utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa upande wa Zanzibar Makamo wa Pili wa
Rais anatoa taarifa na upande wa Tanzania bara Waziri Mkuu atatoa
taarifa ili kujua Chama na Serikali wamefanya nini kwa wananchi na
zinajadiliwa na kuhojiwa,”, alieleza Vuai na kuongeza kuwa endapo
viongozi hao watashirikiana kikamilifu wataweza kupunguza kwa haraka
changamoto zinazowakabili wananchi Majimboni.
Alieleza
kwamba viongozi hao waliochaguliwa na wananchi, wanatakiwa katika
utekelezaji wa Majukumu yao kuhakikisha wanawashirikisha Viongozi wa
Chama wa ngazi mbali mbali ili waweze kutathimini na kuweka kumbukumbu
za kazi hizo kwa usahihi.
Alisema
kila kiongozi aliyetokana na CCM anatakiwa kuendelea kuongozwa na
dhana ya ushindani wa maendeleo ndani ya jimbo lake ili aweze kuaminiwa
na wananchi waliomchagua.
Naibu
Katibu Mkuu huyo, alieleza kuridhishwa kwake na kasi ya kiutendaji ya
baadhi ya viongozi wakiwemo wawakilishi, wabunge na Madiwani katika
maeneo yao na kuwasihi kuendelea kujituma ili kutengeneza tiketi halali
ya kuaminiwa na wananchi waliowapa dhamana za uongozi.
Sambamba
na hayo aliwasihi kujenga utamaduni wa kufanya ziara za mara kwa mara
katika maeneo mbali mbali yaliyopo katika majimbo yao ili kubaini
changamoto sugu zinazowakabili wananchi ili zipatiwe ufumbuzi kwa
haraka.
Alisema
viongozi wa Chama hicho, wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa kwa kila sekta
kwani kufanya hivyo ndio taswira halisi ya ukomavu wa kisiasa wa CCM.
Aidha
aliwapongeza Wajumbe hao wakiwemo Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa
juhudi zao za kufanya kazi kwa bidii katika kuwaletea wananchi maendeo
katika Nyanja mbali mbali za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Alifafanua
kwamba kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kwa baadhi ya
majimbo inaongeza faraja kwa wananchi hasa katika juhudi za kuomarisha
miundo mbinu mbali mbali ikiwemo Ujenzi wa vituo vya afya na ununuzi wa
dawa na ununuzi wa gari za wagonjwa.
Kwa
upande wa sekta ya elimu alizitaja juhuzi za viongozi hao kwamba
wameweza kuimarisha mabanda (madarasa) na kununua bati za kuezekea
sambamba na kununua madawati ili kuwasaidia wanafunzi wakae katika
mazingira bora.
Akizungumzia
sekta ya Miundombinu ya Barabara na Maji alisema baadhi ya viongozi
wameweza kutengeneza barabara za ndani na kushirikiana na serikali
kufikisha huduma za maji kwa wananchi.
Sambamba
na hayo amewashauri viongozi hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu
vikao vyote vya Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge, kwani kupitia
vikao hivyo ndio wataweza kuwasilisha, kuhoji, kushauri na kuitaka
serikali kutatua kwa haraka changamoto zinazowakabili wananchi.
Pamoja
na hayo Naibu Katibu Mkuu Vuai aliwambia viongozi hao kwamba kwa yeyote
atakayetaka ushauri na muongozo wa jambo lolote la kichama, Afisi yake
ipo tayari kumuunga mkono wakati wowote ili kuhakikisha kazi na majukumu
waliopewa na wananchi yanafanyika kwa ufanisi zaidi.

0 comments:
Post a Comment