Na Is-haka Omar, Zanzibar.
WAFUASI wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM ) Zanzibar wameshauriwa kufuata nyayo za waasisi wa Chama
hicho kwa kujitolea na kuweka mbele dhana ya uzalendo katika kujenga
miundombinu ya kudumu itakayowasaidia vizazi vya sasa na vijavyo.
Ushauri huo umetolewa
na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akifungua
kongamano la CCM Wilaya ya Kati Unguja, amesema maendeleo yaliyopatikana
ndani ya serikali na chama yametokana na juhudi kubwa zilizofanywa na
wazee wa chama hicho.
Aliwataka wafuasi wa
CCM kila mtu kwa nafasi yake kufanya jambo la maendeleo litakalobaki
katika vitabu na historia ya kumbukumbu za chama ili vizazi vijavyo
virithi taasisi yenye nguvu katika suala la maendeleo na ukuaji wa
uchumi.
Vuai alisema waasisi
hao wameacha miundombinu na vitega uchumi mbali mbali vikiwemo
miundombinu katika sekta mbali mbali zikiwemo Afya, Elimu na majumba ya
maendeleo yaliyopo kila mikoa nchini ambayo ni matunda ya waasisi wa
muungano na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“ Wazee wetu wamefanya
mengi ambayo ndiyo tunayojivunia kwa sasa katika nyanja mbali mbali za
kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo nasaha zangu na sisi tukiwa Wana CCM
wa zama hizi lazima tubuni mambo mapya yatakayowanufaisha vizazi
vijavyo.”, alieleza Vuai na kuongeza kuwa CCM mpya itajengwa na fikra
mpya zitakazosaidia kuinua maendeo ya chama.
Akizungumzia miaka 40
ya kuzaliwa kwa Chama hicho alisema wananchi wa mijini na vijijini
wameweza kunufaika na fursa mbali mbali zinazotokana na sera za chama.
Alisema wakati CCM
inazaliwa mwaka 1977 ASP ilikuwa na miaka 20 na CCM imetimiza miaka 40
ambayo kwa ujumla wake ni miaka 60 wakati ambao chama hicho kimekuwa
kinara wa Utawala bora na Demokrasia kwa wananchi wa makundi yote.
Aidha, aliwataka
viongozi na watendaji wa Chama na Jumuiya zake kuanzia ngazi za Matawi
kutekeleza kwa vitendo agizo la CCM katika kuadhimisha miaka 40 ya
kuzaliwa kwa taasisi hiyo kwa mtindo wa kufanya shughuli za maendeleo na
ujenzi wa taifa kwa kipindi cha mwaka mzima.
“ Nahitaji kuona ofisi
zetu kuanzia ngazi za Matawi hadi Mikoa kunafanyika shughul za ujenzi
wa taifa zinazoashiria kuzaliwa kwa Chama chetu, na kufanya shughuli za
maendeleo katika Sekta mbali mbali kijamii zikiwemo vituo vya watoto
yatima, Nyumba za kulelea Wazee, Vituo vya Afya na Mahospitalini Unguja na Pemba.”, alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar.
Aliwapongeza Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein
pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pembe
Magufuli kwa juhudi zao za kusimamia kwa uadilifu fursa za kimaendeleo
kwa maslahi ya nchi.
Pia alikiri kuthamini
juhudi zinazofanywa na uongozi wa Chama wa Wilaya hiyo kwa Kusimamia
vizuri utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2020, na
kuwaagiza waendelee kuratibu na kufuatilia kwa karibu shughuli
zinazofanywa na Wawakilishi, Wabunge na Madiwani ndani ya Wilaya hiyo.
Akisoma taarifa ya
utekelezaji wa shughuli za Kisiasa ndani ya Wilaya hiyo, Katibu wa CCM
Wilaya ya Kati Unguja, Ali Yussuf alisema viongozi wa wilaya hiyo kwa
kushirikiana na makada wa Chama wametekeleza shughuli za ujenzi wa taifa
zikiwemo kufanya usafi na mikutano ya ndani ikiwa ni moja ya
shamrashamra za kuzaliwa kwa CCM.
Katibu huyo alifafanua kuwa Wilaya hiyo imejipanga kikamilifu katika kukabiliana na chaguzi za Kichama
na jumuiya kwa lengo la kupatikana viongozi makini na wenye sifa za
kuvusha salama jahazi la CCM katika uwanja wa kisiasa.
Hata hivyo amesema
wanaendelea na ziara maalum kunzia ngazi za mashina hadi Wilaya kwa
lengo la kukagua hali ya kisiasa na kuratibu changamoto zinazowakabili
wananchi wa maeneo mbali mbali ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu kupitia mamlaka husika.
0 comments:
Post a Comment