NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR.
MKURUGENZI wa Chuo Cha Utumishi wa Umma (IPA) Zanzibar , Harusi Ali Masheko amewataka Wanafunzi wa
Vyuo Vikuu , Watumishi wa Umma na Binafsi kutumia kwa vitendo mafunzo
mbali mbali wanayopewa chuoni hapo kama nyenzo ya kuongeza ufanisi wa
kiutendaji katika utekelezaji wa majukumu yao .
Rai hiyo ameitoa wakati akifunga mafunzo ya Siku mbili ya Itifaki za masuala ya Diplomasia na Maslahi ya Taifa yaliyofanyika katika chuo hicho kilichopo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema kupitia
mafunzo hayo washiriki wamepata faida ya kutambua masuala mbali mbali ya
Taratibu na miongozo ya Kidiplomasia hasa katika utatuzi wa migogoro
mbali mbali inayojitokeza nchini ikiwemo ya ardhi na kisiasa.
Alieleza faida
za mafunzo hayo zitaonekana endapo washiriki watatumia kwa vitendo
ujuzi walioupata katika maisha yao ya kila siku na sehemu zao za kazi na
vyuoni kuhakikisha Zanzibar inapiga hatua za kimaendeleo katika Nyanja
mbali mbali za kiuchumi na kijamii.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kutumia miongozo waliopata kupitia mafunzo hayo kujenga dhana ya uzalendo wa kweli katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vinavyotokea nchini.
“ Chuo chetu kitaendelea kutoa mafunzo mbali mbali ya kuwajengea uwezo watendaji mbali mbali wa umma na binafsi pamoja na wanafunzi kulingana na mahitaji yetu kitaaluma.”, alisema Mkurugenzi huyo.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya maendeleo ya Vijana
ya Chuo hicho(IPAUNC), Mohamed Alian alisema jumuiya hiyo imekuwa
ikiratibu mafunzo mbali mbali ya kuinua taaluma za watendaji na
wanafunzi wa vyuo vikuu ili kuhakikisha Zanzibar inakuwa na wataalamu
wenye weledi katika masuala ya itifaki na Diplomasia za kimataifa.
Alitoa pongezi kwa
chuo na Walimu walioshiriki katika uwasilishaji wa Mada mbali mbali
zilizotolewa chuoni hapo, na kuahidi kuwa kutokana na michango, maswali
na mijadala iliyotolewa imeonyesha ishara ya ufahamu kwa washiriki hivyo
wataweza kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Akizungumza mshiriki
wa mafunzo hayo Pandu Salum Sungura, amesema changamoto inayowakabili
vijana wengi wa Zanzibar ni ukosefu wa uzalendo hivyo kupitia mada hiyo
washiriki hao wataifikisha vizuri taaluma hiyo kwa jamii.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyoratibiwa na Jumuiya ya IPAUNC yamejumuiya
washiriki 120 kutoka taasisi za vyuo vikuu, watumishi wa Umma na
Binafsi na zimetolewa mada mbali mbali zikiwemo utatuzi wa migogoro,
uzalendo, masuala ya Usalama wa Taifa na Itifaki za Diplomasia za
kimataifa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment