Zanzibar
RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amelipongeza Jeshi
la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kwa kuendelea na kazi kubwa ya kuilinda Tanzania
pamoja na mipaka yake yote.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya
Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa
ajili ya kujitambulisha rasmi kwa Rais.
Dk. Shein katika
maelezo yake alimueleza Jenerali Mabeyo kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananachi Tanzania
(JWTZ), limeweza kujijengea sifa kubwa ndani na nje ya Tanzania kutokana na
uwezo wake mkubwa unaoenda sambamba na nidhamu na heshima iliyojengeka ndani ya
Jeshi hilo.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa ana imani na matumaini makubwa na uongozi wa Jenerali Mabeyo kuwa
Jeshi hilo litaendelea kuimarika na litafanya mambo makubwa na kumuahidi kua ataendelea
kutoa ushirikiano wake pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili Jeshi
hilo lizidi kupata maendeleo.
“Nakuthibitishia kuwa
tokea siku ulioapishwa nimepata matumaini makubwa kutokana na uongozi wako,
kwani katika uongozi wangu tokea nikiwa Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania nimefanya kazi na Wakuu wa Majeshi watatu na wewe utakuwa wanne na
nimefanya kazi nao vizuri hivyo na wewe nakuahidi kuwa nitaendelea kufanya kazi
vizuri na kukupa mashirikiano yote”,alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliendelea kutoa pongezi kwa Jeshi hilo kwa kuendelea kulinda amani na usalama
huku akiahidi kuendelea kutoa
ushirikiano wake na Jeshi hilo ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wake kwa Brigedi
ya Zanzibar.
Nae Mkuu wa Jeshi la Ulinzi
Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo alitoa shukurani kwa Dk. Shein na kumueleza
kuwa Jeshi hilo limekuwa likipata mashirikiano makubwa kutoka kwake pamoja na
kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aidha, Jenerali Mabeyo
alimpongeza Dk. Shein na kueleza kuwa ni kiongozi mwenye hekima na busara kubwa
hali ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa katika kuiongoza Zanzibar.
Pia, Mkuu huyo wa
Majeshi aliendelea kumueleza Dk. Shein kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananachi
Tanzania linathamini sana ushirikiano anaoutoa Dk. Shein ikiwa ni pamoja na ushiriki wake kwa
Chuo cha Taifa cha Taifa.
Pamoja na hayo,
Jenerali Mabeyo alimueleza Dk. Shein kuwa Zanzibar imeendelea kutumika kwa
vikao mbali mbali vya viongozi wa Majeshi ya Afrika ukiwemo Mkutano wa viongozi
hao kutoka nchi za SADC kutokana na kuwepo kwa amani na utulivu pamoja na kuwa
na vivutio mbali mbali kwa wageni.
Jenerali Mabeyo
aliteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia, ni Amiri
Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli
tarehe 2 Februari na kuapishwa Februari 6 mwaka huu baada ya aliyekuwa Mkuu wa
Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange kustaafu.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 comments:
Post a Comment