KAZI ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar,
imeanza rasmi jana kwa Kampuni ya Bell Geospace Enterprises Limited ya
Uingereza, kufanya utafiti huo kwa niaba ya Kampuni ya Rak Gas ya Ras
Khaimah.
Akizindua utafiti huo uliofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Abeid Amani Karume mjini Unguja jana, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar,
Balozi Seif Ali Idd alisema kwamba utafiti huo, unafungua milango katika
rasilimali ya mafuta na gesi asilia.
“Kuna watu walikuwa wakisema kwamba Zanzibar hatutachimba mafuta, leo
wananchi wenyewe mnashuhudia kazi inaanza…Zanzibar inaendesha utafiti
wa kwanza kabisa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya utafutaji na
uchimbaji wa mafuta,” alisema Balozi Idd.
Alisema serikali haifanyi mambo kwa kubahatisha na kuwaasa wanasiasa
kuacha kuwapotosha wananchi juu ya suala zima la utafutaji na uchimbaji
wa mafuta na gesi asilia kwani suala hilo halihitaji ushabiki wa
kisiasa.
Makamu wa Pili wa Rais alisema kwamba suala la mafuta na gesi asilia,
sasa linasimamiwa Zanzibar moja kwa moja baada ya Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kufanya marekebisho ya Katiba na kuliondoa suala
hilo katika orodha ya mambo ya Muungano.
Alieleza kuwa kazi hiyo ya utafiti wa mafuta na gesi asilia ni hatua
muhimu katika uchimbaji wa mafuta ambapo inaweza kuchukua miaka mitano
kukamilika kwake kwani ni jambo lenye kuhitaji muda, lakini yapo
matumaini makubwa ya kufanikiwa kwa suala hilo.
“Tunawaomba wananchi wawe na utulivu, wasiwe na hofu yoyote wakati
watakapoiona ndege hii maana itakuwa ikipitapita katika sehemu za bahari
na nchi kavu… itapita chini sana, lakini utafiti unaofanywa hauna
athari yoyote kwa binadamu na hata kwa wanyama na mimea,” alisema Balozi
Idd.
Makamu huyo wa Pili wa Rais alisema kwa muda mrefu, serikali imekuwa
na mazungumzo na Kampuni ya Rak Gas ya Ras Khaimah, ambayo mazungumzo
hayo yamezaa matunda ya kuanza kwa kazi ya utafiti, ambapo pia kampuni
hiyo imekuwa mshirika wa maendeleo wa Zanzibar.
Mtaalamu wa uchimbaji mafuta kutoka Kampuni ya RAK Gas ya Ras
Khaimah, Dk Osama Abdelaal alisema kampuni wanatumaini makubwa ya
kufanikiwa katika utafiti huo.
Kiongozi wa timu ya watafiti kutoka Kampuni ya Bell Geospace
Enterprises Limited ya Uingereza, Stefan Kuna akitoa maelezo mafupi
kuhusu kazi ya utafiti huo, alisema kwamba watatumia muda wa miezi
mitatu kufanya utafiti huo Unguja na Pemba.
Mtaalamu huyo alisema ndege yao ya utafiti, itakuwa ikiruka kila siku
mapema asubuhi na itakuwa angani kwa muda wa saa sita, wakitafiti
maeneo yote ya nchi kavu ya visiwa Zanzibar vikubwa na vidogo pamoja na
maeneo ya bahari iliyozunguka visiwa hivyo.
Kampuni hiyo ya kigeni inasaidiwa kazi na kampuni ya kizalendo ya
Brunswick Zanzibar Limited, ambayo inahusika na shughuli za uombaji wa
vibali kutoka serikalini kwa ajili ya ufanikishaji wa kazi ya utafutaji
na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia Zanzibar.
Kuanza kwa kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia,
kunaanza baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk Ali Mohammed Shein kutia saini Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa
Mafuta na Gesi Asilia, Novemba mwaka jana.
Kutungwa kwa sheria hiyo kunatokana na masharti ya Kifungu cha Nne
Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia 2015 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ambayo inataja kwamba shughuli za uendeshaji wa mafuta na gesi asilia,
utafanywa Zanzibar kwa kusimamia na kuendeshwa na taasisi kwa mujibu wa
Sheria za Zanzibar.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment