Na Is-haka Omar, Zanzibar.
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka Wabunge na Wawakilishi wa Pemba
kuwekeza katika sekta ya elimu ili kuwasaidia vijana wanaosoma kwenye
shule na vyuo vya elimu ya juu vilivyopo katika kisiwa hicho.
Kauli
hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla Juma
Saadalla “Mabodi” katika mwendelezo wa ziara yake Pemba wakati akikagua
ujenzi wa shule ya Msingi na Sekondari ya Kwale Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema
viongozi hao pamoja na majukumu waliyokuwanayo wanatakiwa kubuni miradi
itakayosaidia kuinua viwango vya elimu kwa vijana mbali mbali waliopo
katika majimbo hayo ili waweze kupata taaluma zinakazowasaidia kujiajiri
wenyewe.
Alisema
endapo kila jimbo litakuwa na wataalamu mbali mbali waliosomeshwa na
viongozi wa majimbo hatua hiyo itaongeza kasi ya maendeleo kwa kupata
wataalamu wa fani mbali mbali watakaohudumu kwenye sekta za umma na
binafsi katika majimbo hayo.
Sambamba
na hayo aliwaagiza Wabunge na wawakilishi hao kuongeza kasi katika
kutatua kero zinazowakabili wananchi ili kwenda sambamba na matakwa ya
Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Dkt.Mabodi
alisema viongozi hao wanatakiwa kuwa wa kwanza kuratibu changamoto
zinazowakabili wananchi kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kama
walivyowaahidi wananchi hao katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
“Elimu
ndio silaha pekee ya kukuza maendeleo ya nchi yetu pia tutakapokuwa na
wasomi wengi wazawa ndio watakaoweza kupanga mikakati endelevu ya kukuza
uchumi wa taifa letu.”, alieleza Dkt. Mabodi.
Pamoja
na hayo amewapongeza wananchi wa shehia ya Kwale Kisiwani Pemba kwa
uzalendo wao wa kushiriki katika shughuli za kijamii zikiwemo ujenzi wa
Skuli ya Kwale ambayo kwa sasa wanasoma watoto wa shehia hiyo na
vitongoji vyake.
Pia
aliwaomba wananchi wa kisiwa cha Pemba kuunga mkono juhudi zinazofanywa
na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali
Mohamed Shein Pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli kwa kusimamia vizuri fursa za kimaendeleo na
kuimarika uchumi wa nchi zote mbili.
Kupitia
ziara hiyo Dkt. Mabodi kwa niaba ya CCM Zanzibar alichangia shilingi
milioni tatu kwa lengo la kusaidia ujenzi wa madarasa ya Shule ya Kwale.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment