![]() |
| Kiongozi wa Uamsho, Shekhe Faridi Ahmed |
Mawakili wa Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na
Mihadhara ya Kiislamu ya Zanzibar (Jumiki), Shekhe Faridi Ahmed (41) na wenzake
tisa wameiomba Mahakama kufuta taarifa ya kukata rufaa ya Mkurugenzi wa
Mashitaka wa Zanzibar (DPP).
Waliomba hayo jana katika Mahakama ya Rufaa Dar es
Salaam mbele ya Jopo la majaji Januari Msoffe, Salum Massati na William Mandia,
wakati wakisikiliza ombi la kutaka rufaa dhidi ya uamuzi wa dhamana
uliotolewa Machi 11 mwaka huu katika Mahakama Kuu ya Zanzibar litupwe.
Katika uamuzi huo, Mahakama ilitengua mwenendo wa
maombi ya dhamana ya washitakiwa pia ilitupilia mbali maombi ya marejeo ya
uamuzi wa Msajili wa Mahakama Kuu uliowanyima dhamana washitakiwa, pamoja na
kukataa pingamizi la awali la upande wa mashitaka.
Ombi hilo lilisikilizwa jana bila washitakiwa kufika
mahakamani, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa katika eneo la Mahakama, ambapo kila
mtu aliyeingia alikaguliwa na mashine ya ukaguzi.
Wakili wa waleta maombi, Salum Toufiq alidai
wameleta ombi hilo kwa kuwa dhamana ni haki kwa washitakiwa na kwa mujibu wa
Katibu ya Zanzibar, kesi za jinai zinatakiwa kusilikizwa na kutolewa uamuzi
haraka lakini wanachofanya upande wa mashitaka ni kuchelewesha kesi.
Hata hivyo, mawakili wanaomwakilisha DPP walidai
Msajili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, aliyesikiliza maombi ya kwanza ya dhamana
ya washitakiwa hao, hakuwa na mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.
Aidha, walidai maombi ya akina Farid si sahihi, kwa
kuwa wameyaleta kwa kutumia kifungu cha Kanuni za Mahakama ya Rufaa ambacho
kinatumika na Mahakama yenyewe.
Jaji Msoffe alipotaka maelezo kama Msajili
aliyesikiliza maombi ya kwanza ya akina Farid alipewa mamlaka na Jaji Mkuu ya
kufanya hivyo, mawakili wa waleta maombi walidai hakuwa nayo.
Wakili Ramadhan Nassib alidai uamuzi uliotolewa na
msajili ulikuwa batili na msajili huyo alichukua kesi bila ya kufuata utaratibu
hivyo haikuwa sahihi na kwamba kilichobaki Mahakama Kuu ni hati ya mashitaka
dhidi ya washitakiwa tu.
Mbali ya Shekhe Farid, waleta maombi wengine ni
Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Mussa, Azan Khalid, Suleiman Juma Suleiman,
Khamis Ali Suleiman, Hassan Bakar Suleiman, Ghalib Ahmada Jum,Abdallah Said na
Fikirini Fikirini.
Shekhe Farid na wenzake walifikishwa mahakamani Oktoba
25 mwaka jana na kusomewa mashitaka chini ya Sheria ya Usalama wa Taifa na
Sheria ya Kanuni za Adhabu na hawakuruhusiwa kujibu mashitaka yao.
Aidha walinyimwa dhamana kwa kuwa DPP aliwasilisha
hati ya kuzuia dhamana yao kwa madai kuwa watahatarisha usalama wa nchi.
Washitakiwa hawakuridhika na uamuzi huo na kuwasilisha maombi ya marejeo ya
uamuzi huo, lakini upande wa mashitaka uliweka pingamizi ukiomba maombi hayo
yatupiliwe mbali.
Jaji Abrahamu Mwampashi alitupilia mbali pingamizi
hilo la upande wa mashitaka, maombi ya marejeo ya washitakiwa na kubatilisha
mwenendo wa maombi ya dhamana kwa Msajili wa Mahakama Kuu.

0 comments:
Post a Comment