Home » » RC Kaskazini Pemba atoa onyo kwa masheha wanaojihusisha na uuzaji karafuu

RC Kaskazini Pemba atoa onyo kwa masheha wanaojihusisha na uuzaji karafuu





Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh Dadi Faki Dadi amewataka Wakuu wa Wilaya ya Wete na Micheweni  kuwaarifu  Masheha kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ununuzi na uuzaji wa karafuu mbichi na kavu na kwamba atakayebainika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria .

Amesema kuwa Serikali ya Mkoa haitamuonea huruma Sheha yeyote ambaye vitendo vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vitabainika kuendeshwa katika eneo lake , na kuwataka kuwa makini katika kulinda uchumi wa Nchi .

Aidha Mh Dadi ,  amesema kuwa watu wanaojihusha na biashara ya magendo ya karafuu wanapaswa kudhibitiwa na kila mwananchi lakini masheha wao wanatakiwa kuzungumza na wananchi wao na kuwapa tahadhari hiyo mapema kabla ya sheria kuchukua mkondo wake .

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa katika kufanikisha udhibiti wa magendo ya karafuu , vyombo vya ulinzi vimejipanga kikamilifu ili kuona hakuna mwanya unaotumika kusafirisha karafuu kwenda nje ya nchi ambapo tayari jeshi la Polisi limeagizwa kuweka vizuizi vya barabarani  (Road Block)  ili kudhibiti wanaosafirisha karafuu kutoka eneo moja kwenda eneo jengine bila ya kufuata taratibu .

Amefahamisha kwamba mwananchi anayetaka kusarifisha karafuu kutoka Shehia moja kwenda nyingine anatakiwa kuwa na kibali kinachomruhusu kufanya hivyo .
Shehia ya Mtambwe Kaskazini katika Wilaya ya Wete bado vitendo vya uuzaji na ununuzi wa karafuu mbichi na kavu kwa njia ya vikombe pamoja na wizi wa karafuu katika mashamba ya wakulima vimekithiri .

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa