Home » » Watendaji Halmashauri watakiwa kufuata taratibu za manunuzi

Watendaji Halmashauri watakiwa kufuata taratibu za manunuzi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ Mh,  Haji Omar Kheir amewataka watendasji wa halmashauri na mabaraza ya miji kusimamia vyema matumizi ya fedha za serikali kwa kufuata sheria na taratibu za manunuzi halisi ya kile kinachonunuliwa .
Amesema kuwa tatizo ambalo limekuwa likitokea katika Idara ka kuwepo na upotevu wa fedha za serikali ni kutokana na kutokuwepo na wataalamu wa kada ya uhasibu na manunuzi katika Idara hizo .
Akizungumza kwa nyakati tofauti na masheha na madiwani na watendaji wa halmshauri na mabaraza ya miji wa Mkoa wa Kaskazini Pemba , amesema kuwa kamwe hatokuwa tayari kuona kuwa fedha za serikali zinatumika kinyume na ilivyokusudiwa na atakuwa tayari kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria .
Amesema kuwa kila mmoja anapaswa kuheshimu sheria  No 5 /2005 ambayo inaongoza suala la manunuzi na matumizi kwa Idara za Serikali na kuwataka kushirikiana pamoja katika utendaji wa kazi lakini sio kwa kufichiana maovu .
Aidha  amewasisitiza watendaji wa baraza na mji na halmashauri kuvitambua vyanzo vyao vya mapato Ili iwe rahisi kuweza kukusanya mapato na kutimiza azma ya ukusanyaji wa mapato ya kutosha kwa mujibu wa malengo ya bajeti zao  .

Mapema akizungumza katika kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh ,  Dadi Faki Dadi amewataka Watendaji wa Serikali katika mkoa huo kila mmoja kwa mujibu wa nafasi aliyonayo , kuwajibika ili kuhakikisha Mkoa kupitia idara au taasisi unapata maendeleo .
Akitoa ufafanuzi juu ya suala la vitambulisho vya mzanzibar mkaazi , amewataka madiwani kutoogopa kuwaambia ukweli wananchi juu ya utaratibu wa kujiandikisha kwenye daftari la sheha ili kuondoa lawama za kutotambuliwa na masheha .
Amesisitiza kwamba suala la vitambulisho ni jambo ambalo kila mwanachi mwenye sifa anahaki ya kupewa ikiwa atafuata sheria  na taratibu zilizowekwa .


0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa