Waziri wa Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto Zanzibar, Zainab Omar
Juma. Waziri huyu anasema jamii ikitoa ushirikano ubakaji utakwisha
Zanzibar.
Imani na ustaarabu wa watu wa Zanzibar vimeanza kupotea.
Sasa eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa matukio ya
ubakaji nchini. Watuhumiwa nao wanaonewa haya kupelekwa katika vyombo
vya sheria, kama makala haya yanavyoeleza.
Maisha ya mtoto Siajabu Abdallah (sio jina lake
halisi), yako mashakani. Woga na wasiwasi vimemzonga akilini, kiasi cha
kushindwa hata kutembea peke yake.
Madhila haya yote yampatayo mtoto huyu wa umri wa
miaka 12, yanatokana na tukio la kinyama alilofanyiwa miezi minne. Ni
tukio la kubakwa ambapo awali mtu aliyemfanyia unyama huo alimpiga kabla
ya kutimiza haja zake.
Siajabu anasimulia kuwa mkasa huo ulimpata
alipokuwa njiani akielekea shuleni. Alikutana na kijana njiani
aliyemkamata kwa nguvu, akamfunga kamba na kisha kutimiza azma yake
iliyomsababishia maumivu makubwa mwilini.
Iliwalazimu madaktari kufanya kazi ya ziada kuokoa maisha ya mtoto huyu aliyeumizwa vibaya katika sehemu zake za siri.
Sasa Siajabu anaendelea vyema kijijini Kiyanga
baada ya kushonwa nyuzi sita sehemu za siri. Lakini ili kwenda shule,
hana imani na usalama wake, analazimika kuongozana na kaka ama dada.
Dada yake aitwaye Mariamu Said Othman anasema kwa sasa mdogo wake hawezi kwenda shule peke yake, lazima aambatane na mtu mzima.
“Ndugu yangu baada ya kubakwa ameathirika kisaikolojia, yaani akimwona mtu yeyote anamwogopa” anasema huku akilia.
Ubakaji Zanzibar
Siajabu ni miongoni mwa watoto kadhaa waliopatwa
na kadhia ya kubakwa katika Wilaya ya Magharibi, huku wahusika
wakishindwa kufikishwa katika mikono ya sheria.
Licha ya kampeni zinazoendelea kupiga vita vitendo
vya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, hali kisiwani unguja siyo
nzuri kwa kuwa vitendo hivyo vinashamiri huku jamii ikionekana kukaa
kimya bila ya kuchukua hatua stahiki.
Viongozi wa Serikali, mitaa, wanaharakati
wanasema vita dhidi ya ubakaji vinakwamishwa na kukithiri kwa rushwa
miongoni mwa watendaji wa vyombo vya sheria na uelewa mdogo wa jamii
kuhusu unyanyasaji kwa watoto.
CHANZO;MWANANCHI
CHANZO;MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment