Home » » Shein: Zingatieni vipaumbele kupanga mipango ta maendeleo

Shein: Zingatieni vipaumbele kupanga mipango ta maendeleo

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
 
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza umuhimu wa Wizara na Idara za Serikali kuzingatia vipaumbele katika kupanga mipango ya maendeleo ya kila mwaka.
Aliyasema hayo jana wakati akihitimisha taarifa ya Thathimini ya Utekelezaji Kazi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2012- 2013 na robo mwaka ya mwaka wa fedha 2013-2014 katika mkutano uliofanyika Ikulu.

Katika maelezo yake kwa uongozi wa Wizara hiyo Dk. Shein alibainisha kuwa lengo la mikutano hiyo ni kufanya tathmini ya namna Serikali inavyotekeleza majukumu iliyojipangia kwa minajili ya kuzingatia na kuangalia utekelezaji wa bajeti na malengo yaliyowekwa.

Alisisitiza umakini katika kuainisha na kupanga vipaumbele katika kila idara katika wizara ili kurahisisha utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa malengo ya mipango ya Serikali huku dhamira kuu ikiwa ni kuongeza ufanisi na tija katika utendaji Serikalini.

Aliipongeza Wizara ya Afya kwa kukamilisha taarifa hizo mbili za utekelezaji kazi za wizara ambazo zimeonyesha kwa mara ya kwanza mbali ya idara na taasisi zake, lakini pia shughuli za wizara hiyo katika kila wilaya za Unguja na Pemba.

Alisifu mafanikio ya kitengo cha benki ya damu kwa kutimiza malengo ya mwaka uliopita kwa zaidi ya asilimia 100, lakini alihimiza kitego hicho kujiwekea lengo la kujitegemea katika shughuli zake.

Rais alizungumzia pia umuhimu wa uwekaji wa takwimu sahihi katika sekta ya afya huku akihimiza ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi katika suala hilo.

 “Ili kupata takwimu sahihi kitaifa hasa wakati wa magonjwa ya miripuko ni muhimu kuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya sekta ya umma na binafsi,” alisema Dk. Shein.

Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, alikieleza kikao hicho kuwa huduma za afya nchini zinazidi kuimairika kutokana na Serikali wakati wote kuwa sikivu katika masuala ya afya.
Duni alisema maoni ya wananchi ni kuwa huduma katika sekta ya afya nchi zinazidi kuimarika pamoja na changamoto zilizopo.

 Akiwasilisha taarifa ya Wizara hiyo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Saleh Jidawi alileleza kuwa katika mwaka wa fedha uliopita jumla ya wagonjwa wa macho 10,558 walichunguzwa na kupatiwa matibabu katika vituo vya afya 32 na vijiji 26 Unguja na Pemba.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa