Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed
Shein, amewahimiza wananchi kujitolea katika kujiletea maendeleo huku
akiwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuziunga mkono jitihada hizo
kwa manufaa yao na Taifa.
Akizungumza katika ufunguzi wa Kituo cha Afya cha
Kajengwa Makunduchi Mkoa wa Kusini Unguja jana alisema, Serikali wakati
wote itaendelea kuziunga mkono jitihada za wananchi za kujiletea
maendeleo.
Dk Shein aliwaeleza wananchi waliohudhuria
uzinduzi huo ambao ni sehemu ya kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi kuwa,
uimarishaji wa huduma za afya ni uamuzi uliofanywa na Chama cha Afro
Shirazi kama ulivyobainishwa katika mkutano wake wa kampeni za uchaguzi
Julai 8 ,1964.
Aliwakumbusha wananchi hao historia ya utoaji
huduma za afya kabla ya Mapinduzi ambayo ilikuwa ya kibaguzi ambapo
wananchi wanyonge hawakuweza kupata huduma hizo lakini hivi sasa jambo
hilo limebaki kuwa historia.
Aliwapongeza wananchi hao kwa kuonyesha moyo wa
kujitolea ambapo ujenzi wa kituo hicho ulianza mwaka 1999 hatimaye
umekamilika na sasa wanaweza kupata huduma za afya kwa urahisi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Dk Idrissa Muslim
Hija aliishukuru halmashauri hiyo kwa jitihada zake za kuhakikisha kituo
hicho kinakamilika na kuahidi kukitunza.
Katika risala yao iliyosomwa na Katibu wa Kamati
ya Maendeleo, Shehia ya Kajengwa,Nassor Simba Hassan alisema wananchi
hao walieleza kuwa kukamilika kwa kituo hicho kumewapunguzia tabu ya
kufuata huduma hizo mbali.
“Tulipata tabu kufuata huduma hii masafa marefu na
ugumu ulizidi kipindi cha mvua na nyakati za usiku kwa mama wajawazito
na watoto,”ilieleza risala hiyo.
Wakati huo huo Zanzibar imesema hakuna ushahidi
wala uthibitisho wowote uliobaini kwamba Upanga wa Dhahabu wa Jumuiya ya
Jeshi la Polisi la Nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) ulipotelea
Zanzibar.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,
Mohammed Aboud Mohammed ameyasema hayo jana wakati akijibu masuali
katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea huko Chukwani
Mjini Unguja
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment