STATE HOUSE ZANZIBAROFFICE OF THE PRESS SECRETARYPRESS RELEASE Zanzibar 15 Disemba, 2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein amesema ni jambo la kujivunia kuona, wakati huu Zanzibar
ikiadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964, vijana wako
mstari wa mbele kuyafurahia, kuyaenzi na kuyaendeleza Mapinduzi hayo.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar amesema
hayo leo wakati alipokuwa akizungumza katika hafla ya kupokea michango
kwa ajili ya kuchangia matembezi ya vijana kuadhimisha miaka 50 ya
Mapinduzi ya Zanzibar yanayoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM–UVCCM
Zanzibar
Katika hafla hiyo ambayo iliyofanyika katika Bwalo la Maafisa wa
Polisi Oysterbay, jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa pia na Makamu wa
Pili wa Rais Balozi Seif Ali iddi jumla ya shilingi milioni 100
zilikusanywa zikiwa ni ahadi na fedha taslim kati ya shilingi milioni
150 zilizokusudiwa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alichangia
jumla ya shilingi milioni 6 na mke wake Mama Mwanamwema Shein alichangia
shilingi milioni 5.
Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja
na marafiki zake alichangia jumla ya shilingi milioni 10.
Dk. Shein aliueleza uamuzi huo wa UVCCM Zanzibar kuandaa matembezi
hayo ambayo yatafanyika katika mikoa yote mitano ya Zanzibar ni
kielelezo cha namna vijana hao wanavyothamini, kuyaenzi na kuyaendeleza
Mapinduzi ya mwaka 1964 ambayo yaliwapa madaraka ya kujitawala wenyewe
wananchi wa Zanzibar.
Ameusifu uongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa kuandaa matembezi hayo
na kueleza kuwa kwa kufanya hivyo wamefuata nyayo za vijana wenzao wa
Chama cha Afro Shirazi ambao chini ya uongozi shupavu wa Jemedari wao
Mzee Abeid Amani Karume walifanya Mapinduzi tarehe 12 Januari,1960 na
kuwakomboa wananchi wa Zanzibar kutoka kwenye ukoloni.
“kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya mwaka 1964 ni jambo
kubwa katika nchi yetu na kwa maendeleo ya watu wetu”alieleza Dk. Shein.
Akizungumza katika hafla hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya
Matembezi hayo Ndugu Machano Othman Said alisema kuwa matembezi hayo
yanatarajiwa kuzinduliwa huko Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba na Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 22 Disemba,
2013 na kuhitimishwa tarehe 5 Januari, 2014 katika viwanja vya Maisara
mjini Unguja ambapo mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa
Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Alieleza kuwa lengo la matembezi hayo ambayo yatajumuisha pia vijana
kutoka Tanzania Bara ni kutoa hamasa kwa wanachama wa UVCCM na wananchi
kwa jumla katika sehemu mblimbali za Unguja na Pemba kuhusu Mapinduzi ya
mwaka 1964 na ambapo vijana watashiriki pia katika shughuli za kijamii.
Naye Mwenyekiti wa UVCCM-Taifa Sadifa Juma Khamis aliwashukuru
washiriki wote wa hafla hiyo na wale ambao hawakuhudhuria lakini
wamewasilisha michango yao kwa kuitikia wito wa kuchangia matembezi
hayo.Aidha amemshukuru Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa
Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Makamu wa Pili wa Rais Balozi
Seif Ali Iddi kwa kuwaunga mkono na kuwapa moyo katika maandalizi ya
matembezi hayo.
Hafla hiyo imehudhuriwa wa watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa CCM
na wakereketwa wa chama hicho wakiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es
Salaam Ramadhani Madabida na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka
Abdu Shaka.
Postal Address: 2422 Tel.:0776 613 015 Fax: 024 2231822
E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz & sjka1960@hotmail.com
0 comments:
Post a Comment