Home » » SIMBA SC YAPEWA NOTI ZA WANAYANGA.

SIMBA SC YAPEWA NOTI ZA WANAYANGA.

 
Kikosi cha Simba kilichoshiriki kombe la Mapinduzi mjini Zanzibar.
Na Juma Mtanda Blog SIMBA ambayo haijapoteza mchezo wowote tangu kuanza kwa Kombe la Mapinduzi, ikiichapa KCCA ya Uganda leo Jumatatu kwenye mchezo wa fainali itachukua mamilioni yaliyotolewa na Yanga. Mechi hiyo itakuwa ‘laivu’ kwenye Azam TV 1.


Yanga ilijitoa kwenye mashindano hayo na kutoa Sh 10 Milioni kama kuomba radhi kwa waandaji halafu ikaishia zake Uturuki kuweka kambi.

Lakini Simba ikishinda kwenye fainali hiyo itachukua Dola 10,000 ambazo ni kama Sh 16 Milioni za Tanzania. Waandaji ni kama wanaongezea kiasi kidogo kwenye fungu la Yanga.

Mechi hiyo itachezwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Amaan wenye nyasi bandia.

Beki tegemeo wa Simba, Donald Mosoti alisema lengo lao ni kupata bao la mapema sana ili kujiwekea mazingira ya ushindi.

“Tukitaka tushinde hapa ni lazima tuwafunge mapema KCCA kutokana na timu waliyonayo, unajua hawa jamaa tulicheza nao katika mechi za kwanza na hatukufungana. Hawa wanatujua na sisi tunawajua.

“Tukiwafunga watachanganyikiwa halafu watakuwa na akili moja ya kurudisha bao huku sisi tukijipanga kuongeza la pili, naongea na wenzangu kuwafahamisha juu ya jambo hili,” alisema Mosoti mwenye umri wa miaka 29.

Hii ni mara ya pili kwa Simba na KCCA kupambana katika michuano hiyo, Januari 3, mwaka huu zilikutana katika mechi ya Kundi B na kutoka suluhu.

Rekodi ya mechi za Simba katika michuano ipo hivi, ukiondoa suluhu yake na KCCA, imezifunga AFC Leopards bao 1-0, KMKM 1-0, Chuoni 2-0 na URA mabao 2-0.

Simba haijapoteza mchezo ingawa fowadi yake bado haitishi kutokana na kutofunga mabao mengi hadi wanaingia fainali wamefunga mabao sita katika mechi tano walizocheza.

Mchezo huo utawakutanisha wakali ambao ni Amir Kiemba wa Simba na Waswa Herman wa KCCA.

Kocha wa Simba Mcrotia, Zdravko Logarusic ametamba kuibuka na ushindi katika mchezo huo na amewatahadharisha wapinzani wake kuwa kama watakuwa makini kumzuia Kiemba basi wachezaji wengine watafunga na kuchukua kombe.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa