Home » » Zanzibar kushirikiana na Italia kuendeleza, elimu, historia

Zanzibar kushirikiana na Italia kuendeleza, elimu, historia

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imesema ipo tayari kushirikiana na serikali ya Italia katika nyanja za elimu na hifadhi ya sehemu za historia kama ilivyo katika sekta nyingine.
Hayo yalisemwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein wakati akizungumza na Balozi wa Italia nchini, Luigi Scotto aliyemtembelea Ikulu mjini Zanzibar jana.

Katika mazungumzo yao, Balozi Luigi alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake imeanzisha mpango wa ushirikiano kati ya Italia na Afrika, ambao umelenga kuimarisha ushirikiano uliopo.

Alisema chini ya mpango huo, Zanzibar inaweza kufaidika katika masuala ya uhifadhi na ukarabati wa sehemu za historia kama vile Mji Mkongwe pamoja na ufundishaji wa lugha ya Kiitaliano hapa nchini.

Kwa upande wake, Dk. Shein alimueleza Balozi Luigi kuwa ukarabati na uhifadhi wa Mji Mkongwe ni suala linalopewa umuhimu mkubwa na serikali hivyo fursa ya kushirikiana na serikali ya Italia katika suala hilo imekuja wakati muafaka.

Alisema mpango wa kufundisha lugha ya Kiitaliano nao ni muhimu na unaweza kutekelezwa kupitia Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza) chini ya Shule ya Kiswahili na Lugha za Kigeni katika chuo hicho. 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa