Home » » CUF chapinga kushindwa kihalali uchaguzi Kiembesamaki

CUF chapinga kushindwa kihalali uchaguzi Kiembesamaki

Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu wa CUF,Salum Bimani.
 
Chama  cha Wananchi CUF, kimepinga kushindwa  kwa  idadi ya kura katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiembesamaki  badala yake kimeeleza kuzidiwa kwa  maarifa, katika uchaguzi huo uliofanyika kumchagua  mwakilishi wa jimbo hilo. 
Akizungumza na wanahabari visiwani hapa jana Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu wa CUF Salum Bimani,  alisema katika uchaguzi huo  chama chake kimeshindwa kwa  mbinu  zilizotumiwa na wapinzani wake wa CCM.

Alizitaja mbinu hizo  kuwa ni  maarifa ya kuwaingiza mamluki katika daftari la wapiga kura.

Alisema CUF ilibaini mapema maandalizi ya fujo na matumizi mabaya ya nguvu za dola ambavyo viliandaliwa na chama tawala kwa lengo la kuwapa ushindi  wasiostahiki na kuwanyima haki yao ya kufanya maamuzi ya demokrasia.

“Upo ushahidi wa kutosha kwamba vikosi vya serikali vilitumika kuwalinda na kuwasafirisha wapigakura batili na  mamluki kutoka sehemu moja kwenda nyingine pasi na hatua yoyote ya kisheria ikieleweka kwamba kufanya hivyo ni kosa la jinai,” alisema Bimani.

 Aliwaambia waandishi kuwa  vikosi hivyo vilithubutu kutishia kwa bunduki dhidi ya baadhi ya wananchi waliopinga mwenendo huo.

 Alisema uchaguzi huo mdogo wa jimbo la Kiembesamaki haukuwa huru wala wa haki hivyo CUF  hauutambui ushindi wa mgombea wa CCM.

 Alifahamisha kuwa Tume ya Uchaguzi Zanzibar haina uwezo wa kusimamia uchaguzi katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa misingi ya haki, demokrasia na uadilifu.

Katika hatua nyingine Jumuiya ya Wafanyabiashara Viwanda na Wakulima (ZNCCIA) ambao ni miongoni mwa waliokuwa waangalizi wa uchaguzi huo waimeipongeza tume ya uchaguzi Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi huo kwa hali ya amani na usalama.

Akizungumza na wana habari Makamo wa Rais wa jumuiya hiyo Ali Aboud Mzee, alisema uchaguzi huo unapaswa kuigwa na kuwa wa mfano katika chaguzi zote zitakazofanyika kwani ulizingatia misingi ya demokrasia.

Alisema jambo la kusikitisha katika uchaguzi huo ni idadi ndogo ya wapiga kura waliojitokeza ikilinganishwa na watu waliosajiliwa , kiasi cha waliofika kupiga kura hakikufikia hata asilimia 50.

Alisema ZNCCIA ilibaini miongoni mwa matukio yaliojitokeza ambayo hayakuleta madhara ni watu wawili kutaka kupiga kura ambao walikuwa na vitambulisho visivyofanana na sura zao , hata hivyo hawakupiga kura.

Alisema tukio jingine ni kuonekana kwa baadhi ya watu kujazana katika kituo kimoja cha kupigia kura na kusema kuwa ni mawakala wa akiba wa CCM  ambao baadhi yao hawakuwa na vitambulisho.

SOURCE: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa