Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Asha Mohammed Omar amesema wananchi wa Pemba, visiwani Zanzibar walitaka serikali mbili na ‘kaserikali kadogo ka nkataba’.
Alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakiwatakii mema Wazanzibari na kwa muda mrefu hakikuwa kinawataka hivyo anashangaa kuona kimekuwa chema kwao leo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti tulifanya mikutano Pemba tukiongozwa na Nahodha (Mjumbe-Shamsi Vuai Nahodha) na wananchi walisema wanataka serikali mbili na kiserikali kidogo cha ‘nkataba’, wanaosema tofauti ni waongo,” alisema Omar akichangia juzi jioni katika mjadala wa Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba.
Alisema anashangaa kuona Chadema na CUF wapo pamoja bungeni na kueleza kuwa, yeye akiwakilisha vijana, wananchi wa Zanzibar hawataki fujo visiwani humo kwani yaliyotokea Januari mwaka 2001 Pemba yalisababisha watu kupoteza maisha na hawataki yarejee.
“Hawa Chadema hawatutaki na wala hawana haja na sisi…kila siku Tundu Lissu humu bungeni anasema, sasa leo nashangaa Wazanzibari wenzangu wanakuja hapa wanakaa pamoja na Chadema wanaungana eti Ukawa,” alisema.
Aidha, alitaka Umoja huo wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuacha mara moja kwenda Zanzibar kwa ajili ya kufanya maandamano na kusababisha fujo kwa Wazanzibari.
“Nawaambia hivi Ukawa, mkome kuja Zanzibar na kufanya maandamano ambayo yanaleta vurugu, nasema hivi sasa vijana wa CCM tupo imara na tupo tayari kwa lolote…hatutaki vurugu Zanzibar tumechoka,” alisema Omar.
Hata hivyo kutokana na kanuni kuzuia lugha ya kuudhi, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Hassan Suluhu alimtaka mjumbe huyo kufuta kauli yake ya kuwaambia Ukawa wakome. Mjumbe huyo alifuta kauli hiyo.
Omar alisema ; “Viongozi wenzetu wa CCM waliwaua kwa mapanga Pemba, huku CUF wakidiriki kuwasusia maiti Pemba, wametunyanyasa wana CCM wa Pemba, tumechoka na hatuogopi, tutasema mchana bila kuogopa vitisho vyao.”
Chanzo:Habari Leo
0 comments:
Post a Comment