Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
ZAIDI ya watu 15,000 watafaidika na mradi wa pamoja baina ya
Jumuiya ya Hifadhi ya Mji Mkongwe na Jumuiya ya ACRA utakaoanza hivi
karibuni ili kuendeleza Mji Mkongwe.
Hayo yalibainishwa na Mohammed Balow, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
uhifadhi Mji Mkongwe (Zanzibar Stone Town Heritage Society) katika
hafla ya kutiliana saini kati yake na Nicola Moganti ambaye ni Mratibu
wa Shirika la Maendeleo la ACRA.
Miongoni mwa watakaofaidika ni Wazanzibari, mafundi ujenzi 400,
watu 75 wasio na ujuzi, wajasiriamali wa sekta ya ujenzi na ambao
wamesajiliwa na jumuiya hiyo.
Mradi huo utaanzisha maabara katika Chuo Kikuu cha SUZA ambapo
utasaidia kufanya utafiti unaohusu malighafi zinazotumika kujenga
majengo ya kihistoria.
Mradi huo pia utasaidia kuandikwa kwa mtaala unaohusu kufanya
matengenezo ya majengo ya kale ambao mtaala huo utatumiwa na Chuo cha
Karume (Karume Institute of Science and Technology) na kufanya mikutano
na wadau mbalimbali kuzungumzia masuala ya urithi na utamaduni yakiwemo
majengo ya kiasili yaliyopo Zanzibar.
Jumuiya ya uhifadhi Mji Kongwe ndio itakayokuwa muhusika mkuu katika
kupanga na kutekeleza shughuli zinazohusu kutoa taaluma na kukuza
uelewa wa masuala ya kihistoria na urithi wa utamaduni uliopo visiwani
humo huku ikiandaa na kufanya kampeni kwa skuli zenye lengo la kutoa
taaluma kwa ajili ya kukuza uelewa juu ya masuala ya urithi na utamaduni
wa Zanzibar.
Mradi huo wa miaka mitatu wenye lengo la kuhifadhi na kutunza urithi
wa utamaduni Zanzibar na kuhifadhi sekta hii kwa kuchangia ukuaji wa
uchumi nchini utagharimu jumla ya EURO 1,200,000.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment