Home » » MILIPUKO YA MABOMU YAZUA HOFU ZANZIBAR

MILIPUKO YA MABOMU YAZUA HOFU ZANZIBAR

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  Jeshi la Polisi lawamani
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein
Kukithiri kwa matukio ya milipuko ya mabomu  Zanzibar likiwamo la juzi lililomuua Sheikh mmoja na kujeruhi waumini wengine wanane, yameibua hofu kubwa kwa wananchi wa visiwani humo.
Tukio hilo la mlipuko ni la nne kutokea mwaka huu, mengine ni pamoja na yale yaliyotokea katika Kanisa la Evangelist lililopo eneo la Fuoni, Machi 2, Kanisa la Anglikana, Mkunazini Februari 24 na hoteli ya Mercury, Forodhani.

Pia kumekuwapo na mtiririko wa matukio ya kumwagiwa tindikali na watu kupigwa risasi visiwani humo.Kutokana na vitendo hivyo vya kinyama, makundi mbalimbali ya watu Zanzibar, yamelaani vikali matukio hayo hususani la kuuawa kwa Sheikh Muhammed Abdallah Mkumbalagula (27) na watu wengine wanane kujeruhiwa katika

NIPASHE jana ilimtafuta IGP Mangu kuzungumzia hali hiyo, lakini alisema alikuwa katika safari eneo la Darajani Ijumaa usiku, baada ya kulipuliwa kwa bomu na watu wasiojulikana.

Cha kuchangaza ni kwamba katika matukio hayo hakuna mtu yeyote aliyekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Matukio yanayotokea Zanzibar ambayo yanahatarisha uvunjifu wa amani ni chokochoko na vurugu zinazofanywa na watu wasiojulikana kwa lengo la kuivuruga amani ya nchi,” alisema kiongozi wa Kanisa la Anglikana, Zanzibar, Mchungaji  Emmanual Masoud, wakati akizungumza na NIPASHE kuhusiana na kasi ya matukio hayo.

Hata hivyo,  Mchungaji Masoud,  alisema ana imani kuwa tukio hilo la mlipuko wa bomu halifungamani na itikadi za kidini na kwamba vitendo hivyo vinarudisha nyuma maendeleo ya nchi ikizingatiwa kwamba Zanzibar inategemea sekta ya utalii.

Alisema, vitendo hivyo kama havitakomeshwa, uchumi wa Zanzibar utaporomoka, huku akiwasihi wananchi kujiepusha na vitendo hivyo ili kuepusha vifo na majeraha kwa watu wasio na hatia.

 Alilitaka Jeshi la Polisi kuongeza nguvu za ziada ili kuwakamata wahalifu, kwani matukio mengi ya uvunjifu wa amani yanayotokea visiwani humo, lakini hakuna wahalifu wanaokamatwa.

 “Jeshi la Polisi wawe wawazi katika shughuli zao. Siwafundishi kazi, ila inavunja moyo matukio mengi yaliyotokea yakiwamo ya milipuko ya mabomu hakuna wahalifu waliokamatwa, lakini pia huwa hawatoi taarifa kwa wananchi kuhusu hatua waliyofikia na nguvu zao huonekana siku za tukio tu,” alisema.

 Naye Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (Jumaza), Muhidin Juma, aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu na wananchi wote wa Zanzibar kutulia na kuviachia vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi zao za uchunguzi.

Aidha, alisema,  waumini wa Kiislamu na wananchi wa Zanzibar wamesikitishwa sana kuhusiana na tukio hilo. 
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema wanachama wa chama hicho wamesikitishwa sana na tukio hilo na kwamba halilengi kuleta mustakabali mwema wa taifa.

“Kwa kweli tukio hili limetia aibu sana katika nchi yetu hasa ikizingatiwa kuwa waumini wa dini ya Kiislamu kutoka nchi mbalimbali wamekusanyika Zanzibar kwa ajili ya kufanya ibada ijulikanayo kwa jina la Ijitimai,” alisema Vuai.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kutulia na kuendelea kudumisha amani na kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kuwafichua wahalifu wa matukio hayo.

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa Chama cha Wananchi (CUF), Salim Bimani, alisema chama hicho kinalaani vikali tukio hilo la kuwahujumu wahadhiri hao ambao walikuwa wakihubiri dini.

Bimani alilitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi yake ya uchunguzi ili kujua chanzo cha tukio hilo na kuwafichua wahalifu wa matukio hayo ambayo yanaitia dosari nchi.

 Hata hivyo, alisema, tukio hilo halifungamani na itikadi za kidini kwani Wazanzibari wote wanaishi kwa pamoja na kila mtu anahubiri dini yake.“Zanzibar ni tulivu, nashangaa, sijui matukio haya yanafanywa na nani maana hata siasa yetu tuliyonayo Zanzibar hatujafikia kulipua mabomu,” alisema Bimani.

Aliwataka wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kupiga vita matukio hayo na kuinusu nchi kukumbwa na majanga. 
 Naye mmoja wa majeruhi wa mlipuko huo, Ahmed Haidar Jabir, ambaye alilazwa katika hospitali ya Alrahma baada ya kujeruhiwa mguu wake, alisema hali yake inaendelea vizuri.

Wakati huo huo, wapelelzi wa Jeshi la Polisi kutoka Dar es Salaam, wamewasili Zanzibar kusaidiana na wenzao katika juhudi za kufanya upelelezi ambao utasaidia kuwakamata wahalifu waliohusika na tukukio hilo.

Makachero hao waliwasili juzi na kuanza kazi mara moja na kwamba  katika uchunguzi  wa awali, taarifa zinasema kuwa wamegundua kuwa bomu lililotumika kufanya uhalifu huo halikuwa la kienyeji kama ilivyodaiwa awali.

NI BOMU LA KIJESHI
“Wapelelezi wenzetu wamefika visiwani hapa na tunaendelea na uchunguzi, mabaki ya bomu yanaonyesha kuwa bomu lililotumika limetengenezwa kiwandani ila uchunguzi unaendelea,” alisema Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam.

Taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na kamanda huyo zilieleza kuwa, bomu hilo ni la kijeshi la kurusha kwa mkono.
Alisema hadi jana hakuna aliyekamatwa, tofauti na taarifa zilizoenea kuwa watu wawili walitiwa mbaroni.

JK: WAHUSIKA NI WAOGA
Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za pole Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kufuatia mlipuko wa bomu ulioua mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.

“Hicho ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani  Bara na Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na hakikubaliki katika dunia ya sasa,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake na kuongeza:

“Hiki ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na ustaarabu wa aina yeyote ile.”
Rais alikemea tabia hiyo na kuwataka watu kuwa wastaarabu, wavumilivu na kuheshimu  imani na mitizamo ya watu wengine hata kama hawakubaliani nao.

Rais alisema amesikitishwa zaidi na watu hao wasio na ustaarabu ambao walifanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya kidini ambako ndipo

mahali panapostahili amani, uvumilivu na unyenyekevu zaidi kwa kuwa ni eneo ambalo binadamu anafanya mawasiliano na muumba wake. Rais Kikwete alilitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya  vyombo vya sheria waliohusika katika tukio hilo .
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa