KATIBU Mkuu wa Chama
cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema chama hicho
kimejipanga ili kuhakikisha kinaweka historia mpya Zanzibar katika
Uchaguzi Mkuu ujao, anaripoti Mwajuma Juma, Zanzibar.
Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar, aliyasema hayo juzi kwenye hafla ya kukabidhi mashine tisa za boti kwa ajili ya matawi ya CUF, Jimbo la Mji Mkongwe, Mjini Unguja.
Mashine hizo zenye thamani ya sh. milioni 36, zimetolewa na Mbunge wa jimbo hilo, Bw. Ibrahim Sanya (CUF), ambaye pia amekabidhi sh.milioni 27 kwa ajili ya ununuzi wa boti.
Alisema chama hicho hakipo tayari kumvumilia kiongozi yeyote ambaye atakiuka taratibu za chama na wabunge walioshindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.
"CUF itafanya uhakiki wa wanachama wote ambao watajitokeza kugombea nafasi za uongozi na kufanyiwa usaili ili kuhakikisha viongozi watakaopewa nafasi ya kukiwakilisha chama hicho katika uchaguzi wanalinda masilahi ya wananchi na chama.
"Nampongeza Bw. Sanya kwa kutekeleza ahadi zake, jambo hili limekijengea heshima chama chetu na kuonesha uaminifu kwa wapigakura, CUF itaendelea kusimamia, kutekeleza ahadi tunazozitoa kwa wananchi," alisema Maalim Seif wakati akihutubia Mtaa wa Mwembe Tanga.
Aliwataka wawakilishi wa chama hicho, kutokutoa ahadi ambazo hazitekelezeki ili wasikivunjie heshima chama hicho na kuongeza kuwa, CUF itahakikisha Uchaguzi Mkuu ujao unafanyika kwa amani na utulivu.
Alisema kama kutakuwa na njama zozote za kuvuruga uchaguzi au matokeo ya uchaguzi huo, hatawajibika kuwashawishi vijana kwa lolote badala yake atawaachia watetee haki yao.
"Mwaka huu sishawishiki hata aje IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi), kuniomba niwaambie vijana wangu, nimeamua kulisema hili ili viongozi wa kitaifa waweze kulijua," alisema.
Kwa upande wake, Bw. Sanya, amewataka wananchi wa jimbo hilo kuzitumia mashine hizo kwa uangalifu ili ziweze kutumika muda mrefu na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Alisema ataendelea kushirikiana na wananchi wa jimbo hilo ili kuwaletea maendeleo na kuahidi kutekeleza ahadi zote alizozitoa kabla ya Oktoba mwaka huu.
Mapema akisoma risala ya wanachama wa CUF jimboni humo, Katibu wa Vijana, Bw. Mahamoud Ali Mahinda, amesema kitendo cha Mbunge huyo kutekeleza ahadi zake kwa wananchi kimekijengea heshima chama hicho, kujenga imani kwa wananchi wa jimbo hilo.
"Mashine hizi pamoja na boti, zinasaidia kuongeza kipato cha wananchi, kupunguza tatizo la ajira kwa vijana," alisema.
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment