Home » » Zanzibar, India zatiliana saini mkataba wa uwakala wa utangazaji Utalii wa ZNZ nchini India

Zanzibar, India zatiliana saini mkataba wa uwakala wa utangazaji Utalii wa ZNZ nchini India


01
Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL ENTERPRISES ya India Nd. Jilesh H. Babla wakitiliana saini mkataba wa makubaliano ya kuanzishwa kwa ofisi ya uwakala wa Utangazaji Utalii wa Zanzibar Nchini India. (Picha na Makame Mshenga Maelezo-Zanzibar).
                                                 Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar                                                         
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar  imetia saini mkataba wa makubaliano ya kuanzishwa kwa ofisi ya uwakala wa Utangazaji Utalii wa Zanzibar Nchini India.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nd. Ali Mwinyikai wakati wa kutia saini Mkataba huo katika ukumbi wa Wizara hiyo iliyopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mkataba huo umetiwa saini tarehe 17/02/2015 na  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Nd. Ali Mwinyikai na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL ENTERPRISES ya India Nd. Jilesh H. Babla.
Katibu huyo amesema kuwa uanzishwaji wa ofisi ya utalii nchini India haukuja kwa bahati mbaya ila ni utekelezaji wa ilani na malengo yaliyopangwa na kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyopo madarakani kwa upande wa sekta ya Utalii kwa lengo la kuitangaza zaidi Zanzibar kiutalii.
Amesema ofisi hizo zitafanya kazi kama mabalozi wa kuutangaza Utalii wa nchi zao kwa kuwapatia habari  watalii wote ambao wana nia ya kuzitembelea nchi husika pamoja na kutoa ushawishi mkubwa utakaowafanya wananchi wa nchi hizo kuwa na maamuzi sahihi ya kuzitembelea nchi hizo.  
02
Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar na kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL ENTERPRISES ya India Nd. Jilesh H. Babla wakikabidhiana mkataba wa makubaliano ya kuanzishwa kwa ofisi ya uwakala wa Utangazaji Utalii wa Zanzibar Nchini India baada ya kumaliza kusaini. 
Aidha Katibu huyo amesema kuwepo kwa ofisi za Utalii nchini India itasaidia kujenga uhusiano mzuri na wa kudumu baina ya Zanzibar na wadau mbalimbali wa Utalii walioko nchini India jambo ambalo linakosekana katika masoko yaliyopo hivi sasa ispokua soko la Itali.
“Tuna kila sababu za Zanzibar nayo kutumia mfumo huu wa utangazaji wa Utalii kwani unaweza kuleta tija kubwa kwa haraka ukilinganisha na mifumo mengine ya utangazaji”, ameeleza Katibu Mwinyikai.
Amesema mpango huo umelenga kuimilikisha Sekta ya Utalii kwa wanachi wote wa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa uwepo wa sekta hiyo unawafaidisha wananchi wa Zanzibar Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni.
Ametanabahisha kuwa kupanuka kwa wigo wa masoko ya Utalii kutaongeza kazi ya utekelezaji wa dhana ya Utalii na kuondokana na utegemezi wa soko la Ulaya ambalo linatishia uhakika wa kuwepo kwake kutokana na athari za Kiuchumi na Kifedha zinazojitokeza siku hadi siku.
03
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar Nd. Saleh Ramadhan Ferouz akijibu maswali ya waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa tukio hilo. 
Nd. Mwinyikai amefahamisha kuwa kutokana na hali hiyo Serikali ya Zanzibar imeamua kuongeza nguvu na kubadilisha mikakati ya utafutaji wa masoko mengine ikiwa ni pamoja na yale yanayochipukia yakiwemo ya Nchi za China, India, Urusi na Uturuki.
Nae mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Jihil Enterprises ya India ambae pia ni mzaliwa wa Zanzibar anaeishi Mumbai India Nd. Jilesh H. Babla amesema ameamua kuwa wakala wa Utalii wa Zanzibar Nchini India kwa lengo la kuitangaza Zanzibar kiutalii kwani Zanzibar ina vivutio vingi vya Kiutalii zikiwemo Fukwe na Mandhari mazuri ya Kisiwa hicho pamoja na sehemu za kihistoria.
Amesema ameamua maamuzi ya kizalendo kuwa Wakala wa Zanzibar Nchini India kwani hadi sasa hakuna wazalendo wanaoishi nje ya Nchi waliyojitikeza kufanya kazi hiyo pamoja na kuvitaka vyombo vya habari Zanzibar kufikisha ujumbe uliyo sahihi kwa wananchi juu ya Utalii wa Zanzibar ili kukuza Utalii wa nchi na hatimae kupelekea kukua kwa uchumi wa nchini.
04
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar ( Kulia),  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JIHIL ENTERPRISES ya India Nd. Jilesh H. Babla ( wa tatu kushoto) na viongozi wengine kutoka Wizara ya Habari pamoja na Kamisheni ya Utalii Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja.(Picha na Makame Mshenga Maelezo-Zanzibar).
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Kamisheni ya Utalii Zanzibar Dr. Ahmada H. Khatib amesema wazo la kuwa na Ofisi ya Utalii Nchini India lilitokana na matokeo ya ziara rasmi ya Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  aliyoifanya Nchini China na India tarehe 27/05/2013 hadi 02/06/2013 ambayo ilijumuisha Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema pamoja na kuwa takwimu za idadi ya watalii wanaotembelea Zanzibar bado zinakumbana na changamoto za kutokuwa sahihi hata hivyo idadi ya sasa inaonyesha kuwa India hutoa watalii zaidi ya 98,000 kwa kila mwaka hivyo ipo haja ya kuwepo kwa wakala wa Utalii wa Zanzibar Nchini humo.
Amefahamisha kuwa makisio ya jumla ya kuendesha Ofisi hiyo Mjini Mumbai, India inakadiriwa kufikia zaidi ya Dola  100,000 za kimarekani kwa Mwaka ambapo Dola zipatazo 27,000 ni za kuendeshea Ofisi hiyo kila mwezi.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa