Na
Anna Nkinda – Maelezo, Mafia
Viongozi wa wilaya ya Mafia na wafanyakazi wa Idara ya afya wametakiwa
kuhakikisha elimu ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) inatolewa kwa
wananchi hii itawasaidia kubadili tabia na kuepukana na ugonjwa huo ambao
maambukizi yake yanazidi kuongezeka.
Mwito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati alipotembelea
Hospitali ya wilaya hiyo na kuongea na viongozi wa Serikali pamoja na na
watumishi wa sekta ya Afya.
Mama
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema
takwimu zinaonyesha maambukizi mapya ya VVU katika wilaya hiyo
yanaongezeka kila mwaka kutoka asilimia 2.2 kwa mwaka 2012 na kufikia asilimia
2.9 kwa mwaka 2014.
“Ni
jukumu letu sote kuhakikisha elimu inatolewa kwa wenyeji wa wilaya hii
kuhusu maambukizi ya VVU, wananchi wajitokeze kwa wingi kupima kwa sababu
huduma hii inapatikana bure katika zahanati 16 na dawa za kupunguza makali
zinatolewa katika zahanati 4”.
Binadamu
ni kiumbe wa kipekee sana kwani Mwenyezi Mungu amempa akili ya kujua mema na
mabaya, leo hii anakuja mgeni hujui mahali alikotoka unakubali kufanya naye
mapenzi matokeo yake unapata ugonjwa wa Ukimwi usio na kinga wala tiba hapo ni
kujitakia lazima hatua za makusudi ziweze kuchukuliwa ili kukabiliana na tatizo
hili”, alisema Mama Kikwete.
Kuhusu
changamoto ya watumishi haswa wauguzi, wakunga na waganga katika wilaya
hiyo aliwashauri viongozi hao kutafuta njia za kuwavutia wauguzi na
waganga, ili wakifika wasiwe na tamaa ya kukimbilia katika wilaya au mikoa
mengine.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema, “Njia hizi siyo lazima ziwe za kuwapa fedha nyingi, bali
kuwatafutia sehemu nzuri ya kukaa, na kuwapatia mazingira bora ya kazi ikiwemo,
kuwepo kwa vifaa tiba na dawa. Mganga akimtibu mgonjwa kisha akapata
nafuu inamtosha kuridhika na kusikia furaha moyoni. Hii peke yake
ni motisha ya hali ya juu”.
Mama
Kikwete pia aliwahimiza viongozi hao pamoja na watumishi wa sekta ya afya
kuwahamasisha wananchi ili wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF)
kwani katika wilaya hiyo ni asilimia 27 tu ya wananchi ndiyo wamejiunga na
huduma hiyo.
“Mfuko
huu pamoja na mfuko wa Taifa wa bima ya Afya (NHIF) ni muhimu sana. Hakuna nchi
duniani inayoendeshwa bila kuwa na bima ya Afya. Bima hizi hamtaziona umuhimu
wake mpaka pale utakapopata dharura ya kuugua au kuuguliwa”, alisisitiza.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndekilo aliwataka wahudumu
hao wa afya kuwanyenyekea na kuwatumikia wananchi kwa moyo wa uaminifu jambo
ambalo litapunguza malalamiko kwani hakuna mjadala katika afya ya mtu.
Mhandisi
Ndekilo alisema kijiografia kisiwa cha Mafia kinatakiwa kujitegemea kwa mambo
mengi na siyo kutegemea nje kama wananchi watapata huduma nzuri ya afya
watatibiwa kisiwani humo na hivyo wagonjwa wa rufaa wa kwenda Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili watapungua.
“Wadau wa Maendeleo wanawapenda wanamafia na wako
tayari kuwasaidia tutashirikiana kwa pamoja ili tuweze kuzitatua changamoto
zinazowakabili kwani afya bora inaleta maendeleo”, alisema.
Kuhusu
Katiba inayopendekezwa alisema Serikali imepeleka nakala za kutosha wilayani
humo hivyo basi watenge muda wa kuisoma na kuielewa ili wakati ukifika
wakaipigie kura.
Akisoma
taarifa ya afya Mganga Mkuu wa wilaya Dkt. Credianus Mgimba alisema kuna
zahanati 16 zinazotoa huduma za uzazi na mtoto kati ya zahanati 18
zilizopo ambapo mbili ni za watu binafsi na hazitoi huduma ya afya ya uzazi na
mtoto. Hakuna kituo cha Afya ila Serikali imetenga eneo la ujenzi katika
kijiji cha Kironge.
Hospitali
iko moja ambayo ni ya wilaya inavitanda 65 na wastani wa wagonjwa wa kulazwa
kwa siku ni 55 katika wodi nne na wagonjwa wa n je (OPD) 250.
Dkt.
Mgimba alisema licha ya Hospitali ya wilaya kuwahudumia wananchi wapatao
50963 kati ya hao wanaume 26126 na wanawake 24837 kutoka visiwa
nane vya Mafia pia inawahudumia baadhi ya wananchi kutoka wilaya za
Rufiji, Mkuranga na Kilwa.
Hii
ni kutokana na jiografia ya bahari na mito kwao ni salama na rahisi zaidi
kusafiri haraka kwenda Mafia kuliko kwenda kutibiwa Hospitali zao
za wilaya na hii huongeza gharama ya kuwahudumia kwani bajeti tutengwa kutokana
na idadi ya wakazi.
“Hali
ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi siyo ya kuridhisha kwani idadi ya wanaoishi
na VVU inaongezeka. Kwa mujibu wa takwimu katika vituo vya kutolea huduma
kwa mwaka 2012 walikuwa wagonjwa 1072 sawa na asilimia 2.2, mwaka 2013 ,
wagonjwa 1378 sawa na silimia 2.7 na mwaka 2014 , wagonjwa 1498 sawa na
asilimia 2.9”.
“Ongezeko
hili linachangiwa na mwingiliano wa wageni toka toka nje ya wilaya na ongezeko
la tabia hatarishi kwa maambukizi mapya ya VVU. Changamoto ni watu wengi
kutojitokeza kupima kwa hiari na unyanyapaa licha ya elimu hiyo kutolewa
mara kwa mara na huduma za upimaji kupatikana”, alisema Dkt. Mgimba.
Alizitaja
changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa watumishi, upungufu wa dawa na
vifaa tiba na mashine za kutolea huduma , kutokuwa na chanzo cha uhakika cha
maji, uchakavu wa chumba cha kuhifadhia maiti na ukosefu wa jokofu, upungufu wa
nyumba za watumishi na kutokuwa na usafiri wa dharula wenye uhakika wa
kuwasafirisha wagonjwa nje ya kisiwa.
Dkt.
Mgimba alisema , “Ili kukabiliana na changamoto hizo tumeweza kuwashawishi
wazawa wenye sifa kwenda kusomea kada ya afya ili wakimaliza warudi na kufanya
kazi katika mazingira waliyoyazoea, kuimarisha ukusanyaji wa fedha za
uchangiaji wa huduma zinazotolewa Hospitalini na zahanati za Serikali, kufanya
matengenezo ya mashine na ukarabati wa majengo kwa awamu kadri fedha
zitakapopatikana.
Naye
Mkuu wa wilaya hiyo Dkt. Nassor Himid ambaye ni daktari wa magonjwa ya wanawake
alisema ili kukabiliana na upungufu wa madaktari atakuwa anafanya kazi
katika Hospitali hiyo kwa masaa mawili kuanzia saa mbili hadi saa nne asubuhi
kila siku pale ambapo hatakuwa na kazi nyingi ofisini.
Dkt.
Himid alisema “Nimeongea na wataalam kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili
watakuja kutoa huduma kwa kipindi fulani na kuondoka pia kukiwa na kazi
ya upasuaji kwa magonjwa ya wanawake nitakuja kufanya kazi hiyo pamoja na kuwa
mimi ni mkuu wa wilaya bado taaluma yangu ya udaktari ipo
palepale”,.
Aidha
Mbunge wa jimbo la Mafia Abdulkarim Hassan Shah alisema kuharibika kwa mashine
za mionzi na Ultrasound katika Hospitali ya wilaya ni tatizo kubwa kwani
ikitokea ajali hakuna vifaa wanalazimika kukodi ndege na kuwakimbiza wagonjwa
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu na vipimo.
“Ajali
nyingi zinazotokea huku ni za pikipiki na watu kudondoka kwenye minazi kwa kuwa
mashine zimeharibika wafanyakazi wa Hospitali hii wanapata lawama nyingi na
kwakuwa wako wachache ukilinganisha na idadi ya wagonjwa hata huduma
zinachelewa. Kupatikana kwa vifaa kutasaidia kuachwa kulaumiwa na wagonjwa
watapata huduma”, Mbunge Shah alisema.
Kutokana
na tatizo la kuharibika kwa mashine za mionzi (X-Ray), Ultrasound na kutokuwa
na genereta la dharula Hospitalini hapo Mjumbe wa Taasisi ya Maendeleo ya
Kisiwa cha Mafia (MIDEF) Dkt. Ramadhan Dau ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) alisema MIDEF watawasiliana na wafadhili
wao ili vifaa hivyo viweze kupatikana.
Dkt.
Dau alisema, “Ninaamini ifikapo mwezi wa tano mwaka huu vifaa hivi vitakuwa vimepatikana
kwani kukosekana kwa mashine za mionzi na ultrasound kunawafanya wananchi
kupata tabu ya matibabu na kulazimika kuingia gharama ya kusafiri
kwenda nje ya kisiwa kupata huduma hii”,.
Wakati
huo huo Mama Kikwete alitembelea shule ya Sekondari ya Micheni nakuongea na
wazazi, walimu na wanafunzi wa shule hiyo.Akiwataka wanafunzi kusoma kwa bidii
na kujiepusha na vitendo vikatavyowapelekea kukatisha masomo yao ikiwemo kupata
mimba katika umri mdogo na ugonjwa wa Ukimwi na kutotimiza ndoto za maisha yao.
Aliwahimiza
wazazi na walimu kusimamia elimu ya watoto wao hii ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha wanakwenda shule na kuhudhuria masomo yao. Pia wasikubali kuwaacha
wakakosa elimu kwa ajili ya ujauzito, wakapata magonjwa ya ngono, wakapoteza
maisha na kuzaa katika umri mdogo.
Mama
Kikwete alisisitiza, “Mnatakiwa kuwa mfano wa kuigwa, kutoa
malezi na huduma rafiki na bora, kuepuka mila na desturi zinazochangia tabia
hatarishi, kujenga na kusimamia nidhamu na kuzungumza na watoto na kuwapa
elimu ya afya na uzazi na stadi za maisha”.
Msisahau
kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili muweze kuichagua
katiba inayopendekezwa na kuwachagua viongozi wakati wa uchaguzi mkuu
utakapofanyika mwishoni mwa mwaka huu pia wanawake jitokezeni kwa wingi
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi”.
Akiongea
kwa niaba ya wanafunzi wenzake dada mkuu wa shule hiyo Nasara Khalifani ambaye
ni mwanafunzi wa kidato cha nne alimkaribisha Mama Kikwete shuleni hapo
na kuzitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa vifaa vya
maabara, kutokuwa na umeme na kutokuwa na maktaba, upungufu wa vitabu vya
masomo ya sanaa na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.
Mama
Kikwete alikuwa wilayani humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na katika
Hospitali ya wilaya aliwaahidi kuwapatia vitanda viwili vya kujifungulia, viatu
vya kuvaa chumba cha upasuaji, kitanda cha kubebea wagonjwa wanaoingizwa chumba
chumba cha upasuaji, kitanda cha upasuaji, mashine ya kutolea dawa za usingizi
na katika shule ya Sekondari Micheni aliwapatia wanafunzi zawadi ya
shilingi laki tano.
Mwisho
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment