Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
LICHA ya kupanda kwa gharama za uendeshaji wa
sekta ya elimu hapa Zanzibar na duniani kote, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kuhakikisha elimu inaendelea kutolewa bure kwa watoto wa Zanzibar
kama ilivyotangazwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, tarehe 23 Septemba,
1964.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameyasema hayo leo huko katika viwanja vya skuli ya Ndijani iliyopo
Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja katika kilele cha Sherehe za kutimiza
miaka 90 tokea kuanzishwa kwa skuli hiyo.
Katika hotuba yake
iliyosema kwa niaba na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar, Mhe. Ali
Juma Shamuhuna, Dk. Shein alisema kuwa uamuzi alioufanya wa kuondoa uchangiaji
wa fedha kwa wazazi katika skuli zote za Msingi za Zanzibar alioutangaza terehe
12, Januari, 2015 katika maadhimisho ya Sherehe za miaka 51 ya Mapinduzi, una
lengo la kuendeleza dhamira hiyo.
Dk. Shein alisema
kuwa amefurahishwa kuona kuwa Wizara ya Elimu inalifanyia kazi agizo hilo na
kuendelea kuwaelimisha walimu na wanafunzi na wazee juu ya madhumuni ya agizo
hilo.
Alisema kuwa
agizo hilo tayari limeshaanza kutekelezwa, ambapo wanafunzi waliomaliza
mitihani yao ya Kidato cha Sita hivi karibuni hawakulipa ada za mitihani na
kuwataka kuongeza jitihada ili wafaulu vizuri mitihani yao.
Aidha, aliwaeleza
wazee kuwa wanawajibu wa kuendelea kuwa karibu na wanafunzi hao ili wawasaidie
na kuweza kuwaelekeza njia bora za kuwajengea misingi imara kwa maisha yao ya
baadae.
Dk. Shein
alisisistiza kuwa, njia bora ya kuzidi kuitunza historia ya Skuli hiyo ni kuhakikisha
walimu, wazazi na wanafunzi wa zamani wa skuli hiyo wanaendelea kushirikiana na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, kwa lengo la kuifanya kuwa ni chimbuko la kutoa watu
maarufu na wataalamu katika nyanja zote wakiwemo viongozi, wanasanyansi, maprofesa,
watafiti na nyota wa wanamichezo mbali mbali.
Pamoja na hayo,
Dk. Shein alieleza kufurahishwa kutokana na skuli hiyo kufanya vizuri katika
michezo mbali mbali, hasa mchezo wa riadha, kwani imeweza kutoa upinzani mkubwa
kwa wanariadha wa Skuli ya Filbert Bai katika mashindano ya Mbio za Nyika,
yanayofanyika kila mara hapa Zanzibar. Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa
pongezi kwa uongozi wa Skuli ya Ndijani kwa kuandaa maadhimisho hayo ya miaka
90 kwa mtindo wa aina yake.
Alisema kuwa
uongozi wa Skuli hiyo pamoja na wananchi wa eneo hilo wameonesha mfano kwa
vitendo juu ya umuhimu wa kuweka kumbukumbu na kuithamini historia ya vijiji,
skuli, taasisi na nchi kwa jumla.
“Mmeweza kuitunza
historia ya skuli hii tokea siku ilipoanzishwa pamoja na kufuatilia maendleo ya
watu waliosoma hapa, kazi mbali mbali walizofanya na nyadhifa muhimu
walizoshiriki Serikalini, katika taasisi binafsi pamoja na Asasi za
Kirai...Nimefurahi kwa uwekaji wenu mzuri wa kumbukumbu. hongereni
sana”,alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo,
Dk. Shein alisema kuwa Sekta ya elimu kama zilivyo sekta nyengine ina historia
kubwa ambayo inapaswa kusomwa na kuifahamu ili kuendelea kuyathamini mafanikio
makubwa yaliopatika katika kipindi hiki cha miaka 51 baada ya Mapinduzi
Matukufu ya Zanzibae ya mwaka 1964.
Dk. Shein alisema
kuwa historia ya skuli ya Ndijani inalingana na historia ya skuli ya Dole
iliyoanzishwa mwaka 1935 na kupewa jina la “Rural Middle School Dole” na Skuli
ya Makunduchi ambayo ilianzishwa zaidi ya miaka 100 iliyopita, akuli ambazo ni
za mwanzo zilizoanzishwa nje ya mji wa Unguja na kutoa fursa kwa wanyonge.
Katika risala ya
wazazi, walimu na wanafunzi iliyosomwa na Mwalimu Saleh Kasim, ilieleza kuwa
skuli ya Ndijani ni miongoni mwa Skuli kongwe hapa Zanzibar iliyojengwa rasmi
mwaka 1925.
Risala hiyo
ilieleza kuwa miongoni mwa viongozi waliosoma skulini hapo ni Mhe. Ali Khamis
Spika wa Kwanza wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Mhe. Samia Suluhu Hassan,
Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban, Mhe.Mtumwa Kheir Mbarouk, Mhe. Haji Makungu
Mgongo, Mhe. Maulid Makame Juma Dk. Issa Haji Zidi, Marehemu Dheikh Mussa
Makungu, marehemu Dk. Dalu na wengineo.
Wananchi hao pia,
aktika risala yao walitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kuiongoza Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mafanikio makubwa, busara na hekima ya hali ya
juu.
Mapema Mhe.
Shamuhuna alitembelea mabanda ya
maonesho ambapo pia katika sherehe hizo kulifanyika mnada na harambee ya vitu
mbali mbali pamoja na kutoa vyeti na zawadi kwa watunukiwa ambapo viongozi
mbali mbali walihudhuria.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
0 comments:
Post a Comment