Na: Khamis Haji (OMKR)
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad
amewahimiza viongozi wa Bandari na viwanja vya ndege Zanzibar kuzidisha
bidii katika utendaji wao na wahakikishe usalama wa wananchi na wageni
wanaotumia maeneo hayo ni wa uhakika.
Maalim
Seif amesema hayo leo wakati alipotembelea uwanja wa ndege wa Zanzibar
na Bandari ya Malindi kufuatilia utekelezaji wa majukumu mbali mbali
katika maeneo hayo, ikiwemo miradi inayoendelea kutekelezwa.
Katika
uwanja wa ndege wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais alipongeza juhudi
kubwa zinazochukuliwa kukamilisha ujenzi wa jengo jipya la abiria
(Terminal 2)
Maalim
Seif amesema mashirika mengi ya ndege ya Kimataifa yameonesha nia ya
kuleta ndege zao Zanzibar, hivyo hatua ya kuwa na uwanja wa ndege wa
kisasa wenye hadhi ya Kimataifa, kama ambavyo litakuwa jengo hilo
litakapokamilika na kuanza kutoa huduma, itaiwezesha Zanzibar kukuza
mapato yake na kujipatia sifa kubwa kitaifa na kimataifa.
Mratibu
wa ujenzi wa jengo hilo, Yassir De Costa amesema jengo jipya
litakapokamilika litakuwa na huduma zote zinazohitajika kwa uwanja wa
ndege wa Kimataifa na litaweza kuhudumia abiria wanaosafiri ndani na
wale wanaoingia na kutoka nje ya nchi.
Aidha,
Maalim Seif amewahimiza viongozi wa Mamlaka ya Anga Zanzibar kuchukua
hatua maalum kuhakikisha Zanzibar inakuwa na wataalamu wengi katika
masuala ya usafiri wa anga, ili kukabiliana na uhaba wa wataalamu hao
uliopo hivi sasa.
Akiwa
katika bandari ya Malindi, Makamu wa Kwanza wa Rais alipongeza hatua
nzuri iliyochukuliwa na Shirika la Bandari kuhakikisha inapunguza
msongamano wa makontena uliokuwepo na kusababisha usumbufu mkubwa,
ikiwemo ukosefu wa nafasi ya kuweka mizigo inayoingia.
Amesema
miongoni mwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Shirika la Bandari ni
kujijengea uwezo wa mawasiliano kati yake na vyombo vyote vinavyo safari
baharini, ili kuweza kubaini kwa haraka pale ajali zinapotokea, na
kuhakikisha sheria zinafuatwa na vyombo vyote vya usafiri wa baharini.
Ameeleza
kuwa Bandari ni eneo muhimu ambalo linahitajika liwe na utaratibu mzuri
unaoeleweka wa ulinzi na usalama, na ni jambo la lazima kwa abiria na
watumiaji wote wa eneo hilo wanafuata taratibu za usalama zilizowekwa
kwa faida yao na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar, Abdallah Juma amesema suala la
ulinzi na usalama limepewa umuhimu wa kipekee katika eneo lote la
Bandari hiyo kazi ambayo wanaifanya kikamilifu kwa ushirikiano na vyombo
vya ulinzi na usalama vilivyopo katika eneo hilo. Katika ziara hiyo ya
siku moja, Maalim Seif alifuatana na Naibu Waziri wa Miundombinu na
Mawasiliano, Mhe. Issa Haji Ussi na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Juma
Malik Akili.
0 comments:
Post a Comment