Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkulima wa karafuu wilaya ya Wete akionyesha matawi ya mkarafuu yaliyokatwa na wezi shambani kwake kwa lengo la kuiba karafuu.
Na Ali Mohamed
SERIKALI
imepiga marufuku uuzaji na ununuzi wa karafuu usio rasmi (vikombe)
kuepusha wizi wa karafuu mashambani na ukataji wa mikarafuu unaofanywa
na baadhi ya watu kutokana na kuzoeleka kwa biashara hiyo.
Wakizungumza
katika nyakati tofauti Wakuu wa Wilaya za Unguja na Pemba wamesema
hakuna ruhusa kwa mtu yoyote kuuza au kununua karafuu mbichi au kavu na
atakaebainika kujihusisha na biashara hiyo atashughulikiwa ipasavyo.
Mkuu
wa Wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdalla alisema tatizo la ununuzi wa
karafuu kwa vikombe, wizi na ukataji wa mikarafuu kwa lengo la kuiba
karafuu lipo.
Alibainisha
kuwa Serikali haiwezi kuvumilia makosa hayo kwa sababu wanaofanya
uhalifu huo hawana imani na Serikali haina imani nao. Alifahamisha kuwa
watakaokamatwa watachukuliwa hatua kwa misingi ya kisheria.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Haji Makungu Mgongo alisema
Serikali ya Wilaya yake kupitia kamati za Ulinzi na Usalama ya Wilaya
kwa kushirikiana na Masheha wataendesha zoezi maalumu la kuwakamata watu
wanaojihusisha na masuala hayo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Alisema
karafuu ni zao la uchumi wa Taifa hivyo Serikali ya Wilaya yake
haitokuwa tayari kuona baadhi ya watu wakihujumu kwa wizi hasa kukata
mkarafuu kwa tamaa ya kupata maslahi ya muda mfupi.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Katibu Tawala wa Wilaya
hiyo Mohamed Omar Hamad alisema wizi wa karafuu ambao pia hupelekea
kukatwa matawi na mikarafuu midogo unawakatisha tamaa wakulima.
Nae
Mkuu wa wilaya ya Wete ambae pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Micheweni
Hassan Khatib Hassan alisema ukataji wa mikarafuu ni uhalifu mkubwa
ambapo tatizo hilo limewahi kuripotiwa ofisini kwake.
Alishauri
kurejeshwa kwa utamaduni wa uchumaji karafuu kwa kambi ambapo Wakulima
na Wafanyabiashara ni vyema wakajenga kambi katika maeneo wanayochuma
karafuu, kufanya hivyo kutapunguza uhalifu unatokea katika mashamba yao.
Wakuu
hao wa Wilaya na baadhi ya Masheha walilishauri Shirika la ZSTC
kuanzishwa dawati maalumu la kufatilia kesi za uhalifu dhidi ya karafuu
na mikarafuu zinazoripotiwa katika vituo vya Polisi.
Mapema
akiwasilisha malalamiko hayo ya wakulima kuibiwa na kukatiwa mikarafuu
yao kwa Wakuu hao wa Wilaya Mkurugenzi wa Mfuko wa Maedeleo ya Karafuu
Ali Suleiman Mussa alisema matatizo hayo yanawaumiza sana Wakulima.
Alisema
wizi wa karafuu na ukataji wa mikarafuu unachangiwa na baadhi ya watu
wanaonunua karafuu mbichi ambapo kisheria ni kosa kwa vile Shirika la
ZSTC ndio Taasisi pekee iliyopewa mamlaka ya kununua na kuuza
karafuu.
Alisema
Shirika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Karafuu umejipanga kufanya
usajili wa wakulima wenye mashamba na wanaokodi karafuu ambapo watapewa
vitambulisho maalumu vya kuwatambua. Alifahamisha kuwa utaratibu huo
utazuia wizi wa karafuu kwa vile wezi hawatokuwa na nafasi ya kuuza
karafuu ZSTC.
Akizungumzia
suala la ubora wa karafuu, Mkurugenzi huyo amewaomba Wakuu hao wa
Wilaya kwa kushirikiana na Masheha kupiga vita uwanikaji usiozingatia
ubora, (uwanikaji kwenye barabara, sakafu na juu ya bati) na kuwataka
Wakulima kuendelea kutumia majamvi kwa shughuli za uanikaji.
Katibu
ambae pia ni Mwanasheria wa Shirika la ZSTC Ali Hilal Vuai
aliwakumbusha Wakuu hao wa Wilaya na Masheha kuwa kukata mikarafuu kwa
ajili ya kuiba karafuu ama kwa matumizi mengine yoyote ni makosa kwa
mujibu wa sheria namba 2 ya Maendeleo ya Karafuu ya mwaka 2014.
Alisema
sheria hiyo inakataza kuihujumu mikarafuu kwa aina yoyote ile na
atakaebainika kufanya vitendo hivyo anapaswa kupelekwa katika vyombo vya
sheria.
Aliwaomba
Wakuu wa Wilaya kupitia Kamati zao za ulinzi na usalama za Wilaya,
Masheha na Polisi Jamii kupambana na vitendo hivyo vya uhalifu dhidi ya
biashara ya zao la karafuu vinavyofanywa na baadhi ya watu wasiokuwa
waaminifu.
0 comments:
Post a Comment