RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwaunga mkono Wawekezaji wa ndani
na nje ya Zanzibar kwa lengo la kukuza na kuuimarisha uchumi sambamba na
maendeleo ya Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema
hayo leo, huko katika kwianda cha Sukari Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja, mara
baada ya kufanya ziara ya kukitembelea kiwanda hicho na kuangalia ukarabati
mkubwa wa majengo pamoja na mitambo yake unaoendelea kufanywa na wawekezaji wa
Kampuni ya Shanta Sugar Holding Lmtd kutoka nchini India.
Katika maelezo yake
Dk. Shein aliueleza uongozi wa Kampuni hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inathamini juhudi kubwa zilizochukuliwa na wawekezaji hao zikiwemo za
kuanza awamu mpya ya kiwanda hicho kwa kutumia compyuta na digital katika
uzalishaji wa sukari na bidhaa nyengine zinazotokana na miwa.
Dk. Shein alisisitiza
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwaunga mkono wawekezaji wa
kiwanda hicho kwani mkakati maalum umewekwa na Serikali kwa kukiimarisha
kiwanda hicho kwa kutambua kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kuimrika
bila ya waekezaji.
“Wawekezaji ni lazima
wasaidiwe ili waweze kuekeza
vizuri”,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kusisitiza haja ya kuimarisha
uhusiano mwema kati ya wawekezaji na Serikali ili na wao wapate faida na
biashara izidi kuwa nzuri huku akieleza matumaini yake kuwa wananchi watapata
nafuu kubwa ya bidhaa hiyo mara uzalishaji utakapoanza kiwandani hapo.
Dk. Shein aliwapongeza
wawekezaji hao kwa kuekeza Dola milioni 30 kwa hatua za mwanzo sambamba na
juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na uongozi wa kiwanda hicho za kuongeza Dola
nyengine milioni 11.5 za Kimarekani katika kukiimarisha kiwanda hicho ambacho
kitakuwa na mitambo ya kisasa na uzalishaji bora wa sukari na bidhaa nyegine
zitokazo na miwa.
Dk. Shein alisema kuwa
juhudi za wawekezaji hao zimemtia moyo
mkubwa ikiwa ni pamoja na azma yao ya kutoa ajira kwa vijana zipatazo 200
katika sehemu za kiwandani na 500 mashambani na kuendelea zaidi ajira hizo kwa
kadri uzalishaji utakavyoimarika.
Pia, Dk. Shein
alifarajika kwa maelezo aliyoyapata kutoka kwa uongozi wa Kampuni hiyo wa
kueleza kuwa watazalisha umeme wao wenyewe ambao watatumia kiwandani hapo na
mwengine kuweza hata kuliuzia Shirika la Umeme la Zanzibar ZECO ili kuweza
kuwasambazia wananchi vijijini.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa maombi yao waliyoyatoa kwake yakiwemo
kuongezewa heka 3500 za ziada, maghala ya kuhifadhia biadhaa zao pamoja na
nyumba za wafanyakazi ambayo yote hayo kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Shein
yatafanyiwa kazi kwa taratibu maalum za serikali.
Dk. Shein aliwapongeza
wawekezaji hao kwa kazi kubwa walizofanya pamoja na hatua kubwa iliyofikiwa
katika uimarishaji wa kiwanda hicho licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza
ambazo zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alitoa rai kwa wawekezaji hao kuitumia vyema mbolea watakayoitoa
kiwandani hapo kwa kuanzisha kilimo cha mboga mboga sambamba na kuwasaidia
wakuma wadogo wadogo ili na wao waweze kuzalisha mbogamboga na kuweza kusaidia
maendeleo ya Zanzibar
Mapema Waziri wa Fedha
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Omar Yussuf Mzee alieleza kuwa
Mradi wa kiwanda hicho ni muhimu sana
kwani utaimarisha uchumi wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa unaunganisha sekta
ya Kilimo hapa nchini.
Mzee alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara yake ya Fedha iliona ipo haja
kubwa ya kuunga mkono Mradi huo kwani utasaidia sana uchumi na maendeleo ya
Zanzibar kwani ni mradi wa Kitaifa na utachangia sana taifa.
Akieleza faida
nyengine muhimu mbali ya uzalishaji wa sukari kutoka kiwandani hapo, Waziri
Mzee alisema kuwa kiwanda hicho kitasaidia suala zima la ajira, umeme, mbolea
na kueleza kuwa katika uzalishaji wa kiwanda hicho hakuna kitakachotupwa.
Nae Mwenyekiti wa
Kampuni hiyo ya uwekezaji Bwana Mahesh Patel alimueleza Dk. Shein hatua mbali
mbali zilizofikiwa na kiwanda hicho katika ukarabati wake mkubwa unaoendelea
huku akimuahidi kuwa kiwanda hicho kitanza kuzalisha sukari mwezi wa Januari mwakani.
Mwenyekiti huyo
alimueleza Dk. Shein miongoni mwa juhudi za ujenzi na ukarabati uliofanyika
ikiwa ni pamoja na ujenzi hodhi la kubwa la maji ambalo litasambaza maji
mashambani, azma ya sukari
itakayozalishwa kiwandani hapo kuwa na kuwa na nembo maalum‘Brand’ ya Zanzibar, unafuu wa
bei ya bidhaa hiyo kwa wananchi wa Zanzibar na mambo mengineyo.
Aidha, Mwenyekiti huyo alieleza kuwa hatua hizo
zilizoanza mwaka jana zimefikia pazuri
na kutumia fursa hiyo kueleza kuwa uzalishaji wa kiwanda hicho utasaidia
uchumi wa Zanzibar sambamba na kuweka historia nzuri ya Zanzibar katika
biashara na uwekezaji huku akitoa pongezi kwa Serikali hasa Wizara yake ya
Fedha kwa mashirikiano mazuri wanayoyapata.
Akitoa maelezo ya utangulizi Mkurugenzi Mtendaji wa
Mamlaka ya Maeneo Huru na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis Nassor, alisema kuwa
ujenzi na ukarabati mkubwa unaoendelea kufanywa na waekezaji hao hasa ikizingatiwa
kuwa zaidi ya mitambo yenye asilimia 80 kiwandani hapo ni chakavu ambayo
itabadilishwa upya una umuhimu mkubwa katika uchumi wa Zanzibar.
Alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa ili haja ya kiuchumi
iweze kutimia hapa Zanzibar na kueleza kuwa muda si mrefu matunda ya kiwanda
hicho yataanza kuonekana
Kambla ya mazungumzo hayo Dk. Shein alitembelea kiwanda
hicho katika maeneo yote na kuangalia hatua za ujenzi zinazoendelea pamoja na
uwekaji wa mitambo mipya, miundombinu ya maji, umeme pamoja na shughuli nyenginezo za kiwanda na
kupata maelezo kutoka kwa viongozi wa kiwanda hicho.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
0 comments:
Post a Comment