Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amevunja
ukimya kwa kusema kuwa alitegemea sana kuwa mgogoro wa kisiasa
ulioibuka Zanzibar, baada ya kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana
ungepelekwa mahakamani.
Mbali na mgogoro huo uliotokana na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha, kufuta uchaguzi huo wa Oktoba 25 kwa
madai ya kuwapo na kasoro nyingi, Jaji Makungu amesema suala hilo pamoja
na mengine ya sheria na katiba yangewasilishwa mahakamani ili kupatiwa
tafsiri sahihi ya vifungu vinavyobishaniwa.
Jaji Makungu alitoa kauli hiyo katika hafla ya kuwakabidhi vyeti
mawakili wapya 47 na hakimu mmoja iliyofanyika katika Mahakama ya
Zanzibar mjini hapa jana.
Alisema cha ajabu ni kuwa masualaa hayo yaliachiwa kujadiliwa
mitaani na katika vyombo vya habari na kuviacha vyombo vya sheria
hususan Mahakama.
“Ningelitoa wito kwenu pale ambapo masuala ya kikatiba na kisheria
yanapojitokeza basi tuyawasilishe mahakamani kwa mujibu wa katiba ya
nchi yetu. Mahakama ndicho chombo pekee kilichopewa mamlaka ya kisheria
ya kutoa tafsiri ya kisheria,” alisema Jaji Makungu.
MGOGORO WA KISIASA ZANZIBAR
Mgogoro wa kisiasa uliibuka Oktoba 28, mwaka jana, baada ya Jecha
kutangaza kufuta matokeo ya urais, uwakilishi na udiwani, akidai kuwa
kulikuwapo na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi katika maeneo kadhaa
hususan ya Pemba.
Awali Oktoba 26, mgombea urais kupitia Chama cha wananchi (CUF)
Malim Seif Sharif Hamad alitangaza kuwa alikuwa ameshinda katika
uchaguzi huo kisha kuwasilisha fomu za matokeo Zec.
Tangazo la Jecha licha ya kupingwa na CUF ambayo ilitaka Maalim
Seif atangazwe mshindi na kuapishwa, pia lilikosolewa na waangalizi wa
kimataifa na wa ndani ambao ripoti zao za awali zilieleza kuwa uchaguzi
huo ulikuwa mzuri kuliko wa mwaka 2010.
Vile vile, nchi kadhaa zikiwamo Marekani, Uingereza na Ireland
ziliitaka Zec kuendelea kutangaza matokeo kwa kuwa ripoti za waangalizi
zilionyesha kuwa ulikuwa uchaguzi huru na haki.
Hali hiyo ilisababisha kufanyika kwa mazungumzo ya kusaka suluhu
yaliyowashirikisha Maalim Seif, mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein;
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na marais wastaafu
wa Zanzibar, Aman Abeid Karume, Ali Hassan mwinyi na Dk. Salmin Amour.
Mazungumzo hayo hata hivyo hayakupata suluhu na Zec kutangaza kuwa
uchaguzi wa marudio utafanyika Machi 20, kwaka huu, ingawa CUF
imetangaza kutoshiriki kwa maelezo kuwa sio uchaguzi halali kwani
ulishafanyika.
Suala lingine ambalo limezua mgogoro ni ukomo wa Serikali ya Umoja
wa Kitaifa (SUK). CUF na makundi mkadhaa wanasema uhaio wa serikali hiyo
ulishamalizika wakati CCM wanasema kuwa Rais na viongozi wengine wa
serikali hiyo bado wako madarakani hadi rais mpya atakapoapishwa.
WITO KWA MAWAKILI
Aliwataka mawakili kutokubali kuburuzwa na wanasiasa kwa kutekeleza
malengo yao kwani mawakili ni watu muhimu sana mahakamani na katika
jamii.
Alisema moja ya misingi ya demokrasia katika nchi ni kuwa na vyama
vingi vya siasa na demokrasia ya mahakama ni kuwa na mawakili.
“Kesi kuwa mawakili kwa pande zote mbili na mawakili hao wakatoa
hoja za kisheria kwa uweledi kunasaidia kufikia uamuzi sahihi, lakini
kesi yenye wakili upande mmoja mara nyingi huonekana kama kesi ya upande
mmoja,” alisema.
Aidha, alisema kesi ambayo haina mawakili inakuwa nyepesi kwa
hakimu au jaji kwa vile wahusika mara nyingi wanashindwa kuibua hoja za
kisheria na wakati mwingine mahakama hulazimika kuibua hoja za kisheria.
“Hivi sasa tuna mawakili wengi, hivyo tujitokeze kuchukua kesi hizi
na tuwasaidie wananchi ambao hawana uwezo mkubwa wa kifedha,” alisema.
Aliwataka mawakili hao kuienzi taaluma ya sheria na kutokubali
ichafuliwe na wanasiasa kwa maslahi yao kwani siasa na uchu wa fedha
ndio maadui wawili wakubwa wanaoiandama taaluma hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ibrahim Mzee
Ibrahim, alisema kuongezeka kwa mawakili ni imani yake kwamba wananchi
wanaohitaji wasaidizi wa sheria watapata fursa zaidi kuwakilishwa.
Naye Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Said Hassan, ambae aliwakilishwa
na Wakili wa Serikali, Mtumwa Said Sandal, alisema kuwa sekta ya sheria
inaendelea kukua siku hadi siku kutokana na kuongezeka wataalamu wa
sheria.
Aliongeza kuwa mawakili wazingatie kuwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984 kwa kuwa ndiyo iliyotoa mamlaka kwa Mahakama kuwa chombo pekee cha
kikatiba chenye mamlaka ya kutekeleza utoaji wa haki.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment