Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Democratic Party (DP), Abdalla Kombo Khamis
Mgombea wa Urais wa Zanzibar kupitia Democratic
Party (DP), Abdalla Kombo Khamis, amejivua uanachama na kutangaza
kutogombea nafasi hiyo baada ya viongozi wa chama hicho Zanzibar
kusimamishwa uongozi kutokana na kupinga kufanyika uchaguzi wa marudio.
Akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, Kombo alisema ameamua
kuchukua uamuzi huo kutokana na viongozi wa juu wa Chama Tanzania bara
kushindwa kuheshimu uamuzi wa viongozi wa Zanzibar wa kususia uchaguzi
huo.
Alisema viongozi wa Zanzibar wana haki ya kukaa, kujadili na kuamua
mambo yanayohusu Zanzibar ikiwamo kushiriki au kutoshiriki uchaguzi wa
marudio, jambo ambalo viongozi wa kitaifa wameshindwa kuheshimu hayo.
Kombo alisema Januari 31 na Febuari 2, mwaka huu, uongozi wa DP
Zanzibar ulikutana na kujadili ajenda ya mkwamo wa uchaguzi na
kukubaliana kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi
20, mwaka huu.
Alisema uongozi wa DP ukiongozwa na Katibu Mkuu Georgina Mtikila,
umepinga uamuzi uliofikiwa na kuwasimamisha viongozi wa Zanzibar akiwamo
Makamu Mwenyekiti, Peter Magwira, na Naibu wake Ramla Faki.
“Mie si Mgombea tena wa urais wa Zanzibar. Nimeamua kujivua
uanachama wangu DP kutokana na kitendo kilichofanywa na viongozi wangu
kupinga chama kususia uchaguzi wa marudio Zanzibar,” alisema Kombo.
Alisema uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa huru na wa
haki na hakuna sababu za msingi za kufanyika uchaguzi wa marudio.
Naye Magwira alithibitisha kuwa amesimamishwa uongozi pamoja na
Faki. Alisema wamepokea barua ya Katibu Mkuu wa DP Febuari 5, mwaka
huu, wakifahamishwa kusimamishwa kwao.
TADEA yakubali, Jahazi hapana
Katika hatua nyingine, uchaguzi huo wa marudio umeanza kuwa
kizungumkuti baada ya chama cha Tadea kimepitisha azimio la kushiriki
huku Jahazi Asili ikiwasilisha barua ya kususia.
Msimamo huo umetangzwa na Katibu Mwenezi wa Tadea Taifa, Rashid
Mshenga baada ya kukamilika kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho
kilichofanyika Magomeni Kondoa, Dar es salaam jana.
Alisema kikao hicho, chini ya Mwenyekiti Liffa Chipaka, kimepitisha kwa kauli moja chama kushiriki uchaguzi wa marudio.
Alisema wameamua kushiriki uchaguzi huo kwa sababu unafanyika kwa
kuzingatia matakwa ya Katiba na sheria ya uchaguzi ya Zanzibar.
Katika uchaguzi uliofutwa matokeo na Mwenyekiti wake, Jecha Salim Jecha, kilimsimamisha Juma Ali Khatib kugombea nafasi hiyo.
Wakati huo huo, mgombea wa urais kupitia Jahazi Asilia, Kassim
Bakar Ali, alisema jana mjini hapa kuwa amewasilisha rasmi barua Tume
ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) juu ya chama chake kutoshiriki uchaguzi wa
marudio.
Alisema kimsingi uchaguzi ulishafanyika hivyo hawaooni sababu ya
kuitishwa uchaguzi mpya na badala yake wakamilishe uchaguzi wa Oktoba
25, mwaka jana.
Alisema kuwa azimio lake limepata baraka zote za chama na kuitaka
ZEC kutotumia picha za wagombea wa chama hicho katika karatasi za
wapigakura, ikiwamo nafasi ya urais.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa ZEC, Salum Kassim Ali, alisema
anajiandaa kutoa taarifa rasmi juu ya vyama vilivyoamua kutoshiriki
uchaguzi huo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment