Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Dk. John Magufuli.
Umoja wa Ulaya (EU), umemgomea Rais Dk. John
Magufuli, kwa kueleza kuwa msimamo wake ni uliotolewa na washirika wa
jumuiya ya kimataifa wa kumtaka kushirikiana na vyama vilivyoshiriki
uchaguzi mkuu visiwani Zanzibar kufikia muafaka.
Akijibu swali la Nipashe kutaka kujua walivyopokea ombi la Rais kwa
jumuiya za kimataifa kuzungumza na CUF, ili wakubali kushiriki uchaguzi
wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, Msemaji wa EU,
Balozi Roeland van de Geer, alisema wanasubiri kuona utekelezaji wa
tamko lao.
"Msimamo wa washirika kadhaa wa jumuiya ya kimataifa nchini, Umoja
wa Ulaya na nchi wanachama wakizungumzia kuhusu uchaguzi wa marudio
kufanyika, umeelezewa bayana kwenye tamko lilitolewa Januari 29, mwaka
huu," alisema Balozi Roeland na kuongeza:
"Mpaka sasa EU hatuna la kuongeza zaidi ya tamko hilo linaloelezea
msimamo wetu kwa ukamili. Hata hivyo, kwa sasa tunaendelea kufuatilia
kwa ukaribu maendeleo yake na tunatumaini maendeleo hayo yataleta habari
njema kwa wote visiwani humo."
Januari 29, mwaka huu, EU jumuiya ya kimataifa inayojumuisha nchi
za Ubelgiji, Canada, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland,
Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden, Uswisi, Marekani na
Uingereza zenye ubalozi nchini, zilitoa tamko la pamoja la kumtaka Rais
kuingilia katika mgogoro huo.
“Tunamtaka Rais Magufuli kuonyesha uongozi wake kupitia mgogoro huu
wa kisiasa kwa kuingilia kati na kutafuta usuluhishi baina ya vyama
vikuu kuhakikisha amani pande zote," ilisema sehemu ya tamko hilo.
Tamko hilo pia lilieleza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuwa
uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka jana, ulikuwa na kasoro zilizoelezwa na
kwamba waangalizi wa kutoka Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU),
Jumuiya ya Afrika Mashariki, EU, Marekani na Jumuiya ya Maendeleo Kusini
mwa Afrika (SADC) waliridhika na mwenendo wa uchaguzi huo.
Walisema wakati mazungumzo baina ya CUF na CCM yakiendelea,
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha,
alitangaza uchaguzi wa marudio.
Tamko hilo lilisisitiza kurejewa kwa mazunguzo ya vyama vinavyovutana na kuwa na maridhiano kuliko kurudi kwenye uchaguzi mpya.
Walisema kurudiwa kwa uchaguzi huo kutaongeza hali ya wasiwasi na
sitofahamu visiwani humo, hivyo ni vyema pande zote (CUF na CCM)
zikakutana na kuwa na makubaliano ya pamoja na ya amani.
"Ili uwe uchaguzi huru na haki ni lazima pande zote zishiriki. Kwa
hali iliyopo kwa sasa itakuwa vigumu kwa waangalizi wa kimataifa
kushiriki uchaguzi wa marudio," lilifafanua tamko hilo.
Mwanzoni mwa Desemba, mwaka jana, waangalizi wa uchaguzi wa Umoja
wa Ulaya (EU EOM) walitoa wito kwa ukamilishwaji wa haraka wa mchakato
wa uchaguzi Zanzibar kulingana na kanuni za uchaguzi shirikishi, za
uwazi, zinazotekelezwa kwa wakati na kuaminika.
Mwangalizi Mkuu wa EU EOM, Judith Satgentini, alisema: “EU EOM iko
tayari kurejea nchini kuangalia mchakato wa uchaguzi Zanzibar pindi
makubaliano ya kuendelea yatakapofikiwa."
Jecha alitoa tamko la kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar Oktoba
25, mwaka jana, baada ya kueleza kasoro tisa zilizojitokeza wakati wa
uchaguzi huo.
Kumekuwa na mvutano baina ya chama tawala (CCM) na chama kikuu cha
upinzani visiwani humo (CUF). Katika mvutano huo, CUF inataka kutangazwa
kwa matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 25, ambao mgombea urais wake, Maalim
Seif Sharif Hamad, alijitangaza mshindi kwa kupata kura 200,007 dhidi ya
178,363 alizopata mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohammed Shein.
Hivi karibuni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga,
alisema: “Baadhi ya watu, mashirika, EU, Marekani, Jumuiya ya Madola na
wote walioona kwamba tume haikutenda haki (Zec kufuta matokeo ya
Uchaguzi wa Zanzibar)… kwamba ingemaliza kuhesabu na matangazo yatoke.
Lakini tume iliona kabisa kwamba ikifanya hivyo itakuwa imekiuka maadili
yake,“ alisema.
“Kwa hiyo kukawa na mvutano. Kwamba kwa upande wa vyama,
walivyopewa maamuzi haya ya tume, wakakaa kuona wafanye nini. Na
tukadhani katika hivi vyama kuzungumza kule, na sisi bara
watatukaribisha, au Serikali ya Muungano watatukaribisha. Lakini
wakasema hata, hili mtuachie sisi wenyewe tutalizungumza kuhusu huu
uamuzi wa tume,” alisema Balozi Mahiga.
“Wengine wakasema hata misaada tunasimamisha, kama vile Marekani
(Fedha za MCC)… tunasimamisha kwa sababu sisi tunaona haya mazungumzo
hayatoi majibu na afadhali tu yatangazwe (matokeo ya uchaguzi) kama
yalivyokuwa, lakini katika hilo baadaye tume ikasema jamani, afadhali
tuite uchaguzi mwingine.
Akijibu baadhi ya hoja za wabunge zilizotolewa wakati wa mjadala wa
Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa 2016/17
Bunge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, alisema Rais
Magufuli hana mamlaka ya kikatiba ya kuingilia masuala ya Zanzibar.
“Kile ambacho baadhi ya wabunge wamekisema hapa ni kama kuitaka
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuingilia mamlaka ya
Zanzibar na tafsiri yake ni kama unataka kuleta hoja ya kujenga serikali
moja,” alisema Masaju.
“Hoja kwamba Rais Magufuli aingilie haiwezekani. Mambo ya ulinzi na
usalama ndio ya muungano na hicho ndicho kinafanyika Zanzibar
kuhakikisha amani na usalama," alisema.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment