BAADA ya Dk Ali Mohammed Shein kutangazwa mshindi kwa zaidi ya
asilimia 90, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hatma ya kuundwa kwa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa itaamuliwa na Rais kwa kufuata matakwa ya
Katiba ya Zanzibar.
Aidha, Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza kutoipa serikali ya
shirikisho itakayoundwa na Rais Mteule Dk Shein kwa kile inachodai kuwa
ushindi wake ni batili ambao umetokana na kubakwa kwa demokrasia.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya
CCM, Waride Bajari Jabu alisema Dk Shein ataongozwa na Katiba ya
Zanzibar pamoja na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika mkutano huo ambao ulikuwa maalumu kwa ajili ya kumpongeza Dk
Shein kuchaguliwa tena kwa mara ya pili na wananchi wa Zanzibar, Jabu
alisema maelekezo yote ya kuundwa kwa SUK yamefafanuliwa kikatiba.
Alisema CCM inaamini kuwa katiba ndiyo msingi wa uendeshaji wa nchi,
hivyo jambo ilo wanaliachia liamuliwe kwa kufuata matakwa husika ya
Katiba ya Zanzibar.
“Rais ataunda serikali yake kikatiba, imefafanua kila kitu,” alisema
Jabu wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari. Katiba ya Zanzibar
ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 inataka Serikali
inayoundwa iwe ya umoja wa kitaifa kwa kuwa na Rais, Makamu wa Kwanza wa
Rais ambaye anatoka chama kikubwa cha upinzani na Makamu wa Pili wa
Rais anayeteuliwa kutoka katika miongoni mwa wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi.
Hata hivyo, katika uchaguzi uliofanyika Jumapili, CCM imeshinda
majimbo yote ya uchaguzi kutokana na hatua ya Chama cha Wananchi (CUF)
kutangaza kutoshiriki katika uchaguzi huo wa marudio.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Dk Shein
alitangazwa kuwa mshindi kwa kupata asilimia 91.4 na mgombea
aliyemfuatia ni wa ADC, Hamad Rashid Mohamed aliyeambulia asilimia tatu
ya kura zilizopigwa.
Kutokana na kutokuwepo mgombea urais aliyepata zaidi ya asilimia 10
ya kura za urais na kutokuwepo kwa chama kilichoingiza wajumbe wengi
Baraza la Wawakilishi, CCM imejikuta inabaki pekee yenye sifa zote
kikatiba.
Jabu pia alituma salamu za pongeza kwa Dk Shein kwa kuchaguliwa tena kuwatumikia Wazanzibari kwa kipindi cha miaka mitano.
Akitoa salamu hizo, Jabu alisema ushindi wa Dk Shein umedhihirisha
namna Wazanzibari wanavyoridhishwa na utendaji kazi wake ikiwa ni pamoja
na kumuamini kwao.
Kwa upande wao, Umoja wa Vijana (UVCCM) umesema ushindi alioupata Dk
Shein ni kielelezo cha kuimarika kwa msingi ya demokrasia Zanzibar na
kukubalika kwa mgombea huyo kwa wapiga kura na wananchi wa Zanzibar.
Kaimu Katibu Mkuu alisema aina ya uongozi wa Rais Dk Shein ni wa
kipekee na kwamba kama angekuwa si mtawala mwenye maarifa mapana na
uvumilivu wa kisiasa serikali hiyo anaamini ingevunjika mapema.
Kwa upande wao, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema
jana badala yake chama hicho kitaendelea kuitafuta haki kwa njia ya
amani na utulivu. CUF pia imewapongeza wananchi wote ambao
hawakujitokeza kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Katika taarifa yake, Mazrui alisema CUF haiyatambui matokeo yaliyompa
ushindi Dk Shein kwa kuwa ni matokeo ya kupikwa ambayo yametangazwa na
Tume ya uchaguzi Zanzibar baada ya kuagizwa na viongozi wa CCM.
“Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha amekamilisha kazi aliyoagizwa
kwa kutangaza kile alichoita matokeo ya uchaguzi wa urais, hatutambui
hicho kinachoitwa matokeo ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20,2016,”
alisema Mazrui.
Chanzo Habari leo
0 comments:
Post a Comment