Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya
kiserikali ya Kanga Meternity Trust (KMT) Dkt. Mohd Hafidh akitoa
maelezo ya taasisi hiyo inavyofanya kazi zake kuhakikisha Mama
wajawazito wanapata huduma bora wanapokwenda kujifungua hospitali Kuu ya
Mnazimmoja katika hafla ya kuwasilishwa Utafiti wa Mradi wa PartoMa
iliyofanyika Hoteli ya Tembo, Forodhani Mjini Zanzibar.
Madaktari bingwa wa Hospitali ya
Mnazimmoja Dkt. Naufal Kassim (kushoto), Dkt. Zaki (kati) na Mwenyekiti
wa KMT Dkt. Mohd Hafidh wakijadiliana jambo wakati wa hafla ya
kuwasilishwa utafiti uliofanywa na Dkt. Anna Maaloe (hayupo pichani)
kuhusu wadi za wazazi za Hospitali ya Mnazimmoja.
Mtafiti kutoka Mradi wa PartoMa
Dkt. Anna Maaloe akiwasilisha utafiti wake juu ya huduma za wodi za
wazazi za Hospitali kuu ya Mnazimmoja katika hafla iliyofanyika Hoteli
ya Tembo Forodhani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Baraza la wauguzi
na wakunga Dkt. Amina Abdulkadir akitoa mchango wake wakati wa
kuwasilishwa utafiti wa huduma za wodi za wazazi za Hospitali kuu ya
Mnazimmoja. Picha na Makam Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Dkt. Ali Salum kwa niaba ya
Mkurugenzi wa Hospitali kuu ya Mnazimmoja akimkabidhi cheti na zawadi
Metroni Mkuu wa Hospitali hiyo kwa kushiriki mafunzo ya kuwajengea
uwezo yaliyoandaliwa na Mradi wa PartoMa katika hafla iliyofanyika
Hoteli ya Tembo.
Wauguzi wa wodi ya wazazi katika
Hospitali Kuu ya Mnazimmoja wakimpa zawadi ya mlango na kasha Dkt. Anna
Maaloe kwa kazi nzuri aliyosimamia ya utafiti wa wodi za wazazi katika
Hospitali ya Mnazimmoja. Picha na Makam Mshenga-Maelezo Zanzibar.
****************
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Mradi wa PartoMa unaoshirikisha
Chuo Kikuu cha Copenhagen nchini Denmark na Hospitali Kuu ya
Mnazimmoja wenye lengo la kuongeza ufanisi na kuwajengea uwezo
wafanyakazi wa wodi za wazazi katika hospitali ya Mnazimmoja
umeanza kuleta mafanikio makubwa.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa
na mradi wa PartoMa kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali
Kanga Martenity Trust (KMT) iliyopo Hospitali ya Mnazimmoja umeonyesha
vifo vinavyotokana na uzazi na vifo vya watoto wanaozaliwa vimepungua
tokea kuanza kwa mradi huo mwaka mmoja uliopita.
Akiwasilisha utafiti uliofanywa
na mradi wa PartoMa ambao uliwashirikisha madaktari, wakunga na
wasaidizi wakunga katika wodi za wazazi, Dkt. Anna Maaloe amesema bado
ni mapema kuthibitisha kuwa mafanikio hayo yanatokana moja kwa moja na
kuwepo mradi huo lakini ufanisi na utaalamu wa wafanyakazi kwenye wodi
za wazazi Hospitali ya Mnazimmoja umeongezeka.
Amesema Hospitali za rufaa, kama
ya Mnazimmoja zinawajibu mkubwa wa kuwa na mafunzo ya mara kwa mara kwa
wafanyakazi waliopo na wanaotegemewa siku za mbele na kuweka miongozo
bora ili kuokoa maisha ya mzazi na mtoto pamoja na wagonjwa wa kawaida.
“Kwa kuliona hilo mradi wa
PartoMa umekuwa ukiandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo madaktari na
watendaji wa wodi za wazazi Hospitali Mnazimmoja siku moja kwa miezi
mitatu baada ya saa za kazi na kuweka miongozo ambapo wafanyakazi
wengi wamekuwa wakishiriki,” aliongeza Dkt. Anna.
Katika utafiti huo Dkt. Anna
amesema imebainika kuwa wafanyakazi wengi wa Hospitali ya Mnazimmoja
wamehamasika kuongeza elimu na ufanisi na hiyo inasaidia katika kuokoa
maisha ya wananchi.
Hata hivyo amesema bado
kunachangamoto katika kutoa huduma bora zaidi katika Hospitali ya
Mnazimmoja ikiwemo uhaba wa wafanyakazi katika wodi za wazazi
ukilinganisha na ongezeko kubwa la wazazi wanaotumia Hospitali hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo
iliyofanyika Hoteli ya Tembo Forodhani, Mwenyekiti wa KMT Dkt. Mohammed
Hafidh amesema utafiti huo ambao ni wa kwanza kufanywa na kuwashirikisha
watafiti wa wazalendo Hospitali ya Mnazimmoja utasaidia kuwa na
taarifa sahihi na za uhakika kwa maendeleo ya Hospitali hiyo.
Amesema lengo la utafiti huo ni
kuwasaidia mama wajawazito kujifungua salama na kwa heshma na kuzuia
vifo vya mama na mtoto ambavyo vinaweza kuzuilika.
Nae Dkt. Naufal Kassim amekiri
kuwepo mtafartoMa na ameshauri madaktari kujipanga kufanya tafiti zaidi
za afya na kuyatumia matokeo ya tafiti zilizopo kwa ukamilifu.
Katika hafla hiyo Dkt. Ali Salum
kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja aliwakabidhi
vyeti madaktari, wakunga na wasaidizi wakunga walioshiriki mafunzo
ya kuwajngea uwezo baada ya saa za kazi bila malipo katika hospitali
hiyo.
0 comments:
Post a Comment