Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed
Shein leo amewaongoza viongozi na wananchi mbali mbali katika kisomo
maalum cha kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ikiwa pia, ni
maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 44 ya kifo chake.
Marehemu
Mzee Karume ambaye pia, alikuwa Kiongozi wa Chama cha Afro-Shirazi
(ASP) na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aliuawa siku ya Ijumaa tarehe 07 April, 1972 saa 12:05 jioni katika
Makao Makuu ya ASP ambayo sasa ni Ofisi Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM)
iliyopo Kisiwandui mjini Unguja.
Katika
maadhimisho hayo yaliyofanyika Ofisi Kuu ya CCM ambako ndipo alipozikwa
marehemu, Dk. Shein na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi
walishiriki kisomo maalum cha kumuombea dua kiongozi huyo ambaye kifo
chake kiliushitua ulimwengu mzima.
Baada
ya kisomo hicho viongozi hao walizuru kaburi la marehemu wakiambatana
na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini ambao walipewa fursa za
kumuombea dua marehemu wakiwa kaburini hapo.
Kisomo
hicho cha kumuombea dua Marehemu Mzee Karume kilihudhuriwa na viongozi
mbali mbali akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Magufuli, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
Awamu ya Sita, Mhe. Amani Abeid Karume.
Viongozi
wengine walihudhuria katika hitma hiyo ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Baraza la
Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid, Mufti Mkuu wa Tanzania Bara Sheikh
Abubakar Zubeir, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji, Sheikh wa
Mkoa wa Dar-es- Salam Sheikh Mussa Salum.
Aidha,
Mama Mwanamwema Shein alihudhuria katika tukio hilo akiungana na akina
mama wengine akiwemo, Mama Fatma Karume na Mama Asha Balozi na viongozi
wengine wanawake wa Kitaifa pamoja na viongozi wa serikali zote mbili na
wakiwemo viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh
kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge, Wawakilishi, Mabalozi wadogo
wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar na wananchi kutoka sehemu mbali mbali.
Kisomo
hicho cha kumuombea dua marehemu Mzee Abeid Amani Karume pia, ni
miongoni mwa maadhimisho ya Siku ya Mashujaa, kilitanguliwa na Qur-an
tukufu iliyosomwa na Ustadh Sharif Muhidin na kuongozwa na Sheikh Jafar
Abdallah kutoka Masjid Noor Mohammad,iliopo Kwa Mchina Mwanzo.
Mara
baada ya hitma hiyo, Sheikh Hamid Masoud Jongo kutoka Tanzania Bara,
alitoa mawaidha yalioendana na maudhui ya kumbukumbu hiyo na kumuelezea
marehemu mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi bora kutokana na
kuwafaa watu waliowengi hapa nchini na kumuombea MwenyeziMungu ampe
makaazi mema Peponi.
Sheikh
Jongo alisema kuwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano zimefaidika
na Muungano huo ulioasisiwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja
na Marehemu Julius Kambarage Nyerere huku Sheikh Jongo akishangazwa na
wale wanaoupinga Muungano huo.
Katika
mawaidha yake hayo alisisitiza umuhimu wa kumuombea dua kiongozi huyo
kutokana na msisitizo na msimamo wa kiongozi wa Waislamu, Mtume Muhammad
(S.A.W) wa kupita makaburi kwa kila mwaka kwa ajili ya kuwaombea dua
wale wote waliouhami Uislamu na kutoa mchango wao mkubwa katika dini
hiyo.
Sambamba
na hayo, Sheikh Jongo alieleza kuwa kutokana na juhudi zake Mzee Karume
ndio zilizopelekea kupatikana uhuru sambamba na kuendelea kuwepo kwa
amani na utulivu hapa nchini.
Mara
baada ya tukio hilo, tukio lililofuata lilikuwa ni kuweka mashada ya
maua katika kaburi la marehemu Mzee Karume kitendo kilichofanywa na
viongozi wakuu pamoja na muwakilishi wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
Tanzania, Meja Jenerali Issa Nassor, wawakilishi wa familia, muwakilishi
wa wazee waasisi Mzee Suleiman Omar pamoja na muwakilishi wa Mabalozi
wadogo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar.
Marehemu
Mzee Karume aliongoza harakati za kupigania uhuru wa Zanzibar hadi
kuongoza Mapinduzi yaliyoung’oa utawala wa Kisultani uliokuwa ukihamiwa
na Serikali ya Kingereza baada ya watawala hao kufanya kila njama za
kuwanyima uhuru wananchi wa Zanzibar.
Mzee
Karume anakumbukwa sana na wananchi wa Zanzibar kwa namna alivyoweza
katika kipindi kifupi cha utawala wake kuleta mageuzi makubwa katika
jamii ya Wazanzibari ambapo alisimamia haki na usawa katika umiliki wa
njia za uchumi kama ardhi na kuondoa kabisa ubaguzi katika elimu, afya,
ajira na kuwapatia wananchi makazi bora sambamba na mambo mengine muhimu
ya kimaendeleo na kimaisha.
0 comments:
Post a Comment