WAKATI mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
walioteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein wakiwa ofisini
wakichapa kazi, mawaziri wa zamani kutoka katika Chama cha Wananchi
(CUF) kilichokuwa kikiunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, hawakushiriki
katika sherehe za kukabidhi ofisi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umegundua kwamba mawaziri wa
zamani wa SMZ kutoka CUF waliokuwa wakiunda Serikali ya Umoja wa
Kitaifa, hawakukabidhi ofisi kwa mawaziri wapya, kama utaratibu wa
kiutendaji wa utumishi unavyoelekeza.
Jumla ya mawaziri sita waliokuwa wakishikilia wizara mbalimbali
katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka CUF, hawakushiriki katika
makabidhiano ya ofisi, hata kwa kuwashirikisha wasaidizi wao, manaibu
mawaziri.
Katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwa ikiundwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na CUF tangu mwaka 2010, baada ya kufikiwa kwa
maridhiano ya kisiasa yaliyowezesha kufanyika kwa Kura ya Maoni, CUF
ilikuwa na mawaziri sita ambao ni Fatma Fereji (Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais), Nassor Ahmed Mazrui (Biashara, Viwanda na Masoko), Said
Ali Mbarouk (Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo), Abdilahi Jihadi
Hassan (Mifugo na Uvuvi), Abubakar Khamis Bakary (Katiba na Sheria) na
Rashid Seif (Afya).
Waziri wa sasa wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Rashid Ali
Juma alisema makabidhiano ya ofisi hiyo ambayo yalikuwa yafanywe na
aliyekuwa Waziri wa wizara huyo, Said Ali Mbarouk kutoka CUF
hayakufanyika na kazi hiyo ilifanywa na aliyekuwa Naibu Waziri, Bihindi
Khamis Hamad.
“Mimi nimekabidhiwa Ofisi ya Wizara ya Habari, Utangazaji na Utalii
na aliyekuwa Naibu wa Wizara hiyo Bihindi na sasa nipo nachapa kazi,
ambapo nimefanya ziara katika baadhi ya idara kujua majukumu ya
kiutendaji ikiwemo changamoto zinazowakabili wafanyakazi,” alisema Juma.
Aidha, Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Amina Salum Ali
alikabidhiwa ofisi hiyo na aliyekuwa Naibu Waziri, Thuwaiba Edikton
Kisasi na idara na taasisi zake zote, ikiwemo Shirika la Taifa la
Biashara (ZSTC).
Amina tayari amefanya ziara kisiwani Pemba na kuangalia maendeleo ya
kilimo cha zao la karafuu na aliwataka wakulima kuongeza uzalishaji wa
kilimo hicho, ambacho bei yake katika soko la dunia ni ya uhakika.
Aliyekuwa Waziri, Mazrui ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF, alisema
waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kutoka CUF,
hawakushiriki katika makabidhiano ya Wizara, kwa sababu hawaitambui
Serikali iliyopo madarakani na pia kwamba wao CUF hawakushiriki katika
uchaguzi wa marudio.
“Msimamo wa Chama cha Wananchi upo wazi na unafahamika kwamba
hatuitambui serikali iliyopo madarakani na ndiyo maana hatukushiriki
katika makabidhiano ya ofisi kwa mawaziri walioteuliwa,” alisema Mazrui.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment