Na Is-haka Omar, Zanzibar.
Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’
ameshiriki katika mazishi ya watoto wanne waliofariki dunia jana (juzi)
baada ya kuingia kwenye gari iliyokuwa sehemu ya maegesho na
likajifunga hali iliyopelekea watoto hao kukosa hewa na kufariki huko
Kidongo Chekundu Unguja.
Marehemu
hao waliotambuliwa kwa majina ya Mwatma Mohamed Malawi (2), Haisam
Mustafa(2), Munawar Ahmed Khamis (3) na Muslim Hamza bakar (2) wote
wamezikwa leo katika maeneo tofauti ya Makaburi ya Mwanakwere na Kiembe
samaki Mbuyu Mnene Unguja.
Akizungumza
mara baada ya maziko hayo Naibu Katibu huyo huko katika makaburi ya
Mwanakwerekwe, alisema CCM imepokea kwa masikitiko na mshituko mkubwa
taarifa ya vifo vya watoto hao na inatoa mkono wa pole kwa ndugu, jamaa
na marafiki wa familia zilizopata msiba huo na kuwasihi waendelee kuwa
wavumilivu kwa kipindi hiki cha msiba huo.
Alisema
watoto hao walitarajiwa kuwa ni miongoni mwa viongozi na wataalamu wa
fani mbali mbali wa baadae hivyo msiba huo umeacha pengo kubwa kwa
familia na taifa kwa ujumla.
Aidha
Dkt. Mabodi aliwataka wazazi na walezi nchini kuwa karibu na watoto wao
kwa kuhakikisha mazingira yanayotumiwa na watoto kucheza yanakuwa
katika hali ya usalama ili kuepuka athari zinazoweza kusababisha
majeraha ama vifo kwa watoto wao.
“
Kwa niaba ya CCM Zanzibar nawaomba wanafamilia wote wawe wavumilivu kwa
kipindi hichi cha msiba huku vyombo vya ulinzi na usalama vikiendelea
kufanya uchunguzi wa kina juu ya kubaini chanzo halisi cha vifo hivi na
kutoa taarifa kwa umma.”, alisema Dkt. Mabodi.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti baadhi ya ndugu na wazazi wa marehemu hao
walifafanua kuwa (jana) juzi majira saa 5:00 asubuhi watoto hao walikuwa
wakicheza katika maeneo ya nyumbani kwao ghafla hawakuonekana mtaani
hali iliyozusha hofu kwa familia za watoto wao na wakachukua juhudi za
kuwatafuta katika maeneo mbali mbali hasa katika bandari na maeneo
mengine kwa kuhofia kuwa wameibiwa na watu wasiojulikana.
Akieleza
zaidi Bw. Ahmed Khamis ambaye ni baba mzazi wa mtoto aliyefariki
ambaye ni Munawar, alidai kuwa katika harakati za kuwatafuta watoto hao
walifanikiwa kuwapata majira ya saa 2:00 usiku wa july 16, Mwaka huu
wakiwa ndani ya gari moja lililokuwa limeegeshwa katika maegesho ya gari
za mtaani ambalo mmiliki wake aliliweka kwa muda mrefu na alikuwa
amesafiri.
Bw.
Ahmed alieleza kwamba baada ya hapo yeye kwa kushirikiana na majirani
mbali mbali walishirikiana kuvunja milango ya gari hilo na kufanikiwa
kuwatoa watoto hao wakiwa wamezimia na kupelekwa hospitali kuu yaMnazi
Mmoja ambapo baada ya kufanyiwa vipimo na madaktari wakaambiwa kuwa
tayari wamefariki dunia kutokana na kukosa hewa kwa muda mrefu.
Kwa
mujibu wa maelezo ya shuhuda mmoja aliyehusika na harakati za kuwatoa
watoto ndani ya gari walipokutwa wamefariki alisema mazingira yake
yanaonyesha kuwa kabla ya watoto hao kufariki walikuwa wakichezea gari
hilo na walipoingia ndani mlango ulijifunga na kushindwa kutoka nje hali
iliyosababisha kukosa hewa na kufariki dunia.
Viongozi
mbali mbali wa serikali na Chama Cha Mapinduzi waliudhuria katika
mazishi hayo wakiwemo Katibu wa Kamati Maalum, Idara ya Itikadi na
Uenezi CCM Zanzibar, Bi. Waride Bakari Jabu, Mbunge wa Jimbo la
Jang’ombe Ali Hassan Omar ‘King’ na Waziri wa Kazi,uwezeshaji, wazee, vijana wanawake na watoto Maudline Castico.
0 comments:
Post a Comment