Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Balozi
wa Tanzania Nchini Uingereza na Ireland Dr. Asha Rose Migiro kushoto
akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliyefika kumtaarifa uwepo wa Kongamano la Uwekezaji katika Sekta ya
Biashara na Uchumi kati ya Nchi hizo mbili.

Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akimkaribisha
Balozi wa Tanzania Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Balozi Mbelwa
Kairuki kuzungumzia fursa za uwekezaji zinaweza kupatikana China kwa
ajili ya Zanzibar.

Balozi
wa Tanzania Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Balozi Mbelwa Kairuki
akimuelezea Balozi Seif fursa za uwekezaji zinazoweza kupatikana
Nchini China kwa ajili ya Zanzibar.(Picha na – OMPR – ZNZ.)
Na. Othman Khamis OMPR.
Balozi
wa Tanzania Nchini Uingereza na Ireland Dr. Asha Rose Migiro amesema
Serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Nchini
humo na Ireland unatarajiwa kuandaa Kongamano la Uwekezaji katika
masuala ya Biashara na Uchumi litakalotoa nafasi kwa Wawekezaji wa Nchi
hiyo kuangalia fursa za kuwekeza Nchini Tanzania.
Hata
hivyo alisema Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika mwaka huu ingawa
hadi sasa bado hayajafikiwa maamuzi ya sehemu gani litakapofanyika
Kongamano hilo kati ya Tanzania au Uingereza.
Balozi
Asha Rose Migiro alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar kumpa taarifa
ya uwepo wa Kongamano hilo.
Alisema
maandalizi ya awali yameanza kuchukuliwa kwa kukutana na washirika wa
suala hilo wakianzia upande wa Zanzibar ili maeneo ambayo Zanzibar
itahitaji kutumia fursa ya kujitangaza kwenye Kongamano hilo.
Balozi
Migiro alifahamisha kwamba mipango iliyowekwa na Mamlaka ya Uwekezaji
Vitega Uchimi Zanzibar {ZIPA}, Sekta za Kilimo, Utalii pamoja na Jumuiya
ya ZATO iliyomo kwenye Mpango Mkuu wa Taifa wa kupunguza Umaskini
Zanzibar {MKUZA} awamu ya Tatu imeonyesha mwanga wa kufanikisha azma
hiyo njema.
Zanzibar
ni Visiwa vinavyojitangaza vyenyewe Duniani kutokana na historia yake
ya Kibiashara Kimataifa kwa karne nyingi zilizopita kiasi kwamba sifa
hizo zinastahiki ziendelezwe kwa manufaa ya Wananchi wake.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
aliupongeza mpango huo utakaosaidia kufungua ukurasa mpya wa Kiuchumi na
Kibiashara kati ya Tanzania na Uingereza na Ireland kwa ujumla.
Balozi
Seif alisema Wawekezaji kutoka Uingereza na Ireland wanaweza kuangalia
maeneo ya kuwekeza Visiwani Zanzibar hasa katika Sekta ya Mafuta na Gesi
Asilia pamoja na uvuvi wa Habari kuu kwa vile wameshapiga hatua kubwa
ya maendeleo katika maeneo hayo.
Mapema
asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana kwa
mazungumzo na Balozi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Jamuhuri
ya Watu wa China Balozi Mbelwa Kairuki aliyefika kumuelezea fursa
mbali mbali zilizopo Nchini China ambazo Zanzibar inaweza
kuzichangamkia.
Katika
Mazungumzo hayo Balozi Mbela Kairuki alisema Zanzibar inastahiki
kwenda mbali zaidi katika ushirikiano wake na Majimbo mbali mbali ya
Jamuhuri ya Watu wa China katika juhudi za kuimarisha Uchumi wake.
Balozi
Kairuki alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba mawazo ya
kufikiria Beijing itamaliza kila kitu kwa sasa yamepitwa na wakati kwa
vile Serikali Kuu yenyewe ya Nchi hiyo imekabiliwa na mambo mengi
inayostahiki kuyatekeleza kwanza kabla ya kufikiria kutoa misaada kwa
marafiki zake.
Alisema
Majimbo la Jamuhuri ya Watu wa China yamefanikiwa kuwa na uwezo mkubwa
Kiuchumi pamoja na njanja nyingi za Uwekezaji kiasi kwamba endapo
Zanzibar itafanikiwa kutumia nafasi hizo inaweza kupiga hatua za haraka
za maendeleo.
Alisema
Sekta ya Utalii ni eneo pana linaloweza kufanikisha Uchumi wa Zanzibar
katika kuwakaribisha Wawekezaji pamoja na Watalii kutoka China ambao
bado hawajatumia vilivyo soko la Afrika.
Balozi
Kairuki alieleza kwamba China hivi sasa iko katika kiwango kikubwa cha
uwekezaji Duniani katika Sekta ya Utalii sambamba na Wananchi wake
kupenda kutembea Nchi mbali mbali Duniani nafasi ambayo inaweza
kulitononosha Taifa iwapo kasi hiyo itaelekezwa Zanzibar.
Naye
kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alizipongeza juhudi kubwa zinazochukuliwa na Balozi Kairuki katika
kutafuta fursa za Uwekezaji Nchini China kwa ajili ya Zanzibar.
Balozi
Seif alimuhakikishia Balozi Kairuki kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar itajitahidi kuchangamkia fursa hizo katika azma yake ya
kuimarisha Uchumi na ustawi wa Wananchi wake.
Hata
hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bado wapo baadhi ya
Watendaji wenye dhamana ya kutoa maamuzi wamekuwa na urasimu wa
kuchelewesha miradi na hatimae Wawekezaji walioamua kuweka vitega uchumi
vyao
Nchini kukata tamaa na kuondoka Nchini.
Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba urasimu ni kitendo kibaya kinachoviza Maendeleo na kudumaza Uchumi wa Taifa.
0 comments:
Post a Comment