RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Kampuni ya ‘Kunshan Asia Aroma
Cooperation Limited” kutoka nchini China kwa uamuzi wake wa kuja kuekeza hapa
Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo
leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka
Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China ambayo
imedhamiria kuekeza katika kiwanda cha Makonyo, kilichopo Wawi Pemba kwa
kushirikiana na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Katika mazungumzo hayo, Dk.
Shein aliihakikishia Kampuni hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa
ushirikiano wake mkubwa kupitia Wizara yake ya Biashara na Viwanda pamoja na
Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kuipongeza Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” chini ya
Mwenyekiti wake Zhou Junxue kwa kusaini Makubaliano ya Awali kati ya Kampuni
hiyo na Shirika la (ZSTC).
Aidha, Dk. Shein
aliueleza ujumbe wa Kampuni hiyo kuwa Kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi ni cha
muda mrefu ambacho kimekuwa kikizalisha mafuta ya aina mbali mbali hivyo,
ushirikiano wa pamoja katika uzalishaji kiwandani hapo kutasaidia kuinua ubora
wa kiwanda sambamba na kuongeza pato la Taifa na soko la ajira.
Alieleza kuwa uwamuzi wa
Kampuni hiyo ni mzuri na umekuja katika wakati muwafaka ambapo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, hivyo
hatua hiyo itakuwa chachu katika kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na viungo vya vyakula vya aina
nyingi ambavyo miongoni mwao vimekuwa vikitoa mafuta bora ambayo yamekuwa ni
bidhaa muhimu iliyoingia katika soko la ndani na nje ya Tanzania yakiwemo
mafuta ya makonyo, mafuta ya karafuu na mafuta ya mikaratusi.
Hivyo, Dk. Shein
aliongeza kuwa kuanza kwa uwekezaji huo kutazidi kuitangaza Zanzibar na kuwa
kiwanda cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinachozalisha
bidhaa hizo za mafuta.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alieleza haja ya Kampuni hiyo kushirikiana na ZSTC katika kutekeleza
makubaliano hayo yaliotiwa saini hapo jana ikiwa ni pamoja na kuongeza zaidi
uzalishaji huku akisisitiza suala zima la ufanyaji utafiti katika kilimo cha
mazao hayo yanazotoa mafuta.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza suala la mafunzo ambalo litasaidia sana kuendesha kiwanda hicho
pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za aina mbali mbali za mafuta ya viungo
kutoka katika kiwanda hicho cha Makonyo Wawi jambo ambalo pia, litaongeza soko
la ajira hapa nchini.
Nae Mwenyekiti wa
Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya China, Zhou Junxue
alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar
kwa kupitia sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vidogo na vya kati.
Mwenyekiti wa Kampuni ya
“Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” alimueleza Rais Dk. Shein mikakati
iliyowekwa na Kampuni yake katika kuhakikisha makubaliano waliyosaini
yanatekelezwa kwa lengo la kuleta manufaa kwa pande zote mbili.
Junxue alimuhakikishia
Rais Dk. Shein kuwa Kampuni yake itatoa mashirikiano makubwa kwa Serikali
kupitia Shirika lake la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuhakikisha
kiwanda hicho kinatoa mafuta yalio bora sambamba na kuongeza uzalishaji wa
bidhaa zitakazozalishwa katika kiwanda hicho cha Wawi.
Kampuni ya “Kunshan Asia
Aroma Cooperation Limited” ya nchini China ambayo ndio mnunuzi mkubwa wa mafuta
ya viungo vya Zanzibar tokea Julai mwaka 2017, ilitiliana saini Makubaliano ya
Awali na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuendesha mradi
ndani ya miaka kumi utaohusisha uimarishaji wa utendaji na utaalamu katika
kiwanda cha Makonyo Wawi.
Jambo jengine ni uendelezaji
wa mazao ya karafuu na mikaratusi ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 60
zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia tani 2,000,
ubadilishanaji uzoefu
kati ya watendaji wa taasisi hizo, upatikanaji wa mafunzo, mbinu na upatikanaji
mbegu bora za mikaratusi ni miongoni mwa
makubaliano hayo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
0 comments:
Post a Comment