Home » » Mtuhumiwa kesi ya mauaji Padri Mushi amkataa Jaji

Mtuhumiwa kesi ya mauaji Padri Mushi amkataa Jaji

Mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar,Abdalla Juma
Wakili wa mtuhumiwa wa mauaji ya Padri Evaristus Mushi wa Kanisa Katoliki Zanzibar, amewasilisha ombi la mteja wake la kumkataa Jaji Mkusa Isaac Sepetu, kuendelea na kesi hiyo kwa madai ya kutokuwa na imani naye.
Ombi hilo liliwasilishwa na Wakili Abdalla Juma katika Mahakama Kuu Zanzibar jana, akidai mteja wake hana imani na Jaji Sepetu na kutaka ajiondoe kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Alisema kutokana na mwenendo wa kesi unavyokwenda, mteja wake haamini kama Jaji huyo atatenda haki.

Alisema Machi 28, mwaka huu aliwasilisha ombi dhidi ya Jeshi la Polisi kumshikilia mteja wake kwa zaidi ya saa 24 bila ya kumfikisha mahakakani na kutaka mteja wake aachiwe huru kama polisi wameshindwa kukamilisha upelelezi kwa wakati.

Alisema alikosa imani mapema baada ya Jaji huyo kuendesha kesi yake pamoja na ombi hilo, jambo ambalo alidai mteja wake alikuwa na wasiwasi maombi hayo na kesi yake mojawapo halitafanikiwa kwa vile yote yapo kwa Jaji mmoja.

Wakili huyo pia alidai kuwa mteja wake alidhani Jaji huyo atajitoa kwenye jambo mojawapo ili haki itendeke, lakini hakufanya hivyo na kulitupilia mbali ombi la mteja wake.

Mapema, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Abdallah Mgongo, aliomba mahakama kuahirisha kesi hiyo kutokana na kuwa upelelezi unaendelea kwa kupeleka vinasaba kwa Mkemia Mkuu Dar es Salam na kufuatilia mitandao ya simu.

Jaji Sepetu aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 16, mwaka huu kwa kutolea maamuzi baada ya kupokea ombi la kutakiwa kujiondoa.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa