Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema
haitamvumilia mfanyabiashara yeyote atakayebainika kuingiza bidhaa zilizopita
muda wa matumizi au zilizo chini ya viwango zinazoweza kuathiri afya za
wananchi au kuharibu mazingira.
Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej, huko ofisini kwake Migombani,
alipokuwa akitoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari juu ya hatua ya serikali
kuuharibu unga wa ngano tani 780 ambao uliingizwa Zanzibar ukiwa haufai kwa
matumizi.
Waziri Ferej alisema serikali itaendelea kuchukua
hatua za kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa nchini zinakuwa na ubora na zinazingatia
viwango vinavyostahiki ambazo hazitaweza kuleta madhara kiafya kwa watumiaji na
kimazingira.
Akizungumzia unga wa ngano ulioharibiwa, Ferej
alisema unga huo uliingizwa Zanzibar April mwaka jana na kampuni ya Bopar
Enterprises ukitokea nchini Uturuki ukiwa kwenye makontena 30 ambapo baada ya
kufanyiwa uchunguzi wa kawaida ulibainika haufai kutumiwa na binaadamu.
Alisema baadaye Bodi ya Chakula na Dawa ilipiga
marufuku uingizaji na usambazaji wa unga huo na kuwaagiza wamiliki na
wasafirishaji wa unga huo kuurejesha unakotoka haraka kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, waziri alisema kulitokea mabishano
baina ya wamiliki wa unga huo na kampuni iliyousafirisha iitwayo Mediterranean
Shipping Company; mabishano ambayo yalipelekea unga huo kukaa kwa muda mrefu
katika bandari ya Malindi.
Alieleza kuwa unga huo mbali na uchunguzi hata kwa
macho ulikuwa na fangasi na funza ambapo pia ulianza kuhatarisha afya za
wafanyakazi wa eneo la bandari ya Malindi na watumiaji wa eneo hilo.
Alisema baada ya serikali kuona mvutano huo
unaendelea huku afya za wananchi zikiwa hatarini, iliingilia kati na
ilishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambapo iliamuliwa unga huo
ukaharibiwe Tanzania Bara, kwa vile Zanzibar hakuna eneo la kutosha kwa kazi
hiyo.
Waziri Ferej alisema mwezi Juni mwaka huu makontena
30 ya unga huo wa ngano yalipelekwa Dar es Salaam katika tanuri la kiwanda cha
saruji cha TPCC kilichoko Tegeta, ambako unga huo ulichanganywa na mchanga na
kuharibiwa.
“Kwa furaha naomba nichukue fursa hii kutoa taarifa
kuwa unga mbovu tani 789 uliokuwa umeingizwa Zanzibar umeshaharibiwa,” alisema
Waziri Ferej.
Alisema gharama zote za uteketezaji wa unga huo
jumla ya sh 64,153,500 ambazo zimelipwa na kampuni iliyoleta unga huo Bopar
Enterprises na Miditerranean Shipping Company Limited.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment