Home » » ZANZIBAR WAMPA JK MASHARTI SITA NI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA

ZANZIBAR WAMPA JK MASHARTI SITA NI KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA

 KAMATI ya Maridhiano Zanzibar, imemshauri Rais Jakaya Kikwete kutosaini muswada wa mabadiliko ya katiba na badala yake urejeshwe bungeni kujadiliwa upya kuondoa vifungu vilivyoingizwa kibabe. Hilo ni mojawapo kati ya masharti sita yaliyotangazwa na kamati hiyo ikimtaka Rais Kikwete ayazingatie kabla ya kusaini muswada huo kuwa sheria na kuruhusu mchakato wa Bunge Maalum la Katiba na kura ya maoni kufanyika. Msimamo huo ulitangazwa kwa pamoja na viongozi wa kamati hiyo na Baraza la Katiba Zanzibar (Bakaza) walipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana. Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hassan Nassor Moyo alisema kwamba marekebisho ya muswada huo yamefanyika bila ya kuzingatia maslahi ya pande mbili za Muungano, baada ya wadau kutoka Zanzibar kunyimwa haki ya kujadili muswada huo. Alisema kwamba serikali na Kamati ya Bunge na Katiba, wakati wa kuandaa muswada huo wananchi wamepigwa chenga kwa kunyimwa nafasi ya kuujadili zikiwemo asasi za kiraia visiwani Zanzibar. Moyo alisema kabla ya rais kusaini muswada huo, mambo sita yanahitaji kufanyiwa kazi ikiwemo wadau kupewa nafasi ya kutoa maoni yao na urudishwe upya bungeni kujadiliwa na kupitishwa kabla ya kuwa sheria.
 


Alifafanua kuwa kifungu kinachotoa nafasi kwa wabunge wa Bunge la Katiba kuipitisha kwa wingi wa kura kama utaratibu wa theluthi mbili utashindikana, ufutwe na kubakia utaratibu wa theluthi mbili kama ilivyokuwa awali. Alisema kwamba viongozi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wana umuhimu mkubwa katika kufanikisha kazi ya Bunge la Katiba pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kushiriki kura ya maoni badala ya kazi hiyo kufanywa na tume za uchaguzi pekee. Aidha, kamati hiyo imependekeza wajumbe wa Bunge la Katiba wapatikane kwa idadi sawa baina ya Zanzibar na Tanzania bara kwa vile katiba inayopitishwa imetokana na mataifa mawili yaliyokuwa na sifa sawa kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. “Wabunge 166 wa Bunge Maalumu la Katiba kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na asasi za kiraia wachaguliwe na makundi na taasisi zenyewe badala ya rais,” alisema Moyo ambaye aliambatana na katibu wa kamati hiyo, Ismail Jussa Ladhu. Vile vile, alisema kamati yake inaunga mkono ushauri wa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, baada ya kuwataka wanasiasa na wanaharakati kukaa pamoja kuzungumza matatizo yaliyojitokeza badala ya kufanya maandamano. Naye Mwenyekiti wa Bakaza, Profesa Abdul Shariff alisema marekebisho yaliyofanyika katika muswada huo yana kasoro kubwa katika kupata katiba inayotokana na matakwa ya wananchi badala ya vyama vya siasa. Alisema kwamba kutokana na CCM kuwa na uwakilishi wa asilimia 72 katika Bunge Maalumu la Katiba, upo uwezekano mkubwa wa katiba mpya kutawaliwa na matakwa ya kisiasa kwa kuwa chama hicho tayari kimeweka msimamo wake kuhusu muundo wa Muungano kinyume na mapendekezo ya rasimu ya katiba. “Tunapendekeza wabunge wa Bunge Maalumu wangechaguliwa na wananchi kwa kazi maalumu ya kuandika katiba tu, ili kupata ridhaa yao kuhusu aina ya katiba wanayotaka wakati huu,” alisema.
TANZANIA DAIMA

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa