Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha
Nahodha aliyasema hayo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwishoni mwa wiki, huku NLD ikitawanya taarifa kwenye vyombo vya habari kuilaumu SUK kwa kutochukua hatua za kisheria dhidi ya ufisadi wa fedha za Serikali uliobainika.
Nahodha aliyewahi kuwa Waziri Kiongozi wa SMZ kwa miaka 10 kwenye utawala wa Rais mstaafu Dk. Amani Abeid Karume, alisema jumla ya Shilingi bilioni 60 zimebainika kutafunwa na watendaji wasio waadilifu katika awamu hiyo, na hakuna hatua za kisheria zilizochukuliwa hadi sasa.
Katika mkutano huo uliofanyika Baja, eneo la Ziwani Polisi mjini hapa, Nahodha alionekana kushangaa, akitaja jumla ya Shilingi bilioni 20 kuwa zimepotea kizembe katika Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco), huku Shilingi bilioni 40 zikifisidiwa katika mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.
“Fedha hizi ni nyingi sana, zingesaidia kupungua matatizo kama si kumaliza matatizo yanayowakabili wananchi wanyonge na kutoa huduma muhimu za jamii kama maji safi, afya, elimu na matibabu.
“Lipo tatizo linalohitaji kupiganiwa na kutatuliwa haraka,” alisema Nahodha huku akishangiulkiwa na wananchi.
Alisema kufumbiwa macho watu waliotajwa kuhusika na ufisadi huo ni kwenda kinyume na misingi ya utawala bora wa sheria, na kwamba fedha hizo zingeweza kumudu kuwahudumia wananchi katika maeneo ya mijini na viijini kwa kuimarisha huduma za jamii.
“Inashangaza sana kuona hata wanaojiita wapinzani na wanaharakati Zanzibar wakifumba midomo huku nchi ikiliwa na kundi la watendaji waroho. Kinachofanyika si halali hata kiodogo, hatua za kisheria zinahitajika kuchukuliwa na ukweli ufahamike,” alisema.
Naibu Katibu Mkuu wa NLD-Zanzibar, Khamisi Haji Mussa, alisema chama chake kinahuzunishwa na mwenendo wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kuamua kuunda Tume nyingi na kukosa utekelezaji wa matokeo ya ripoti zake baada ya kuwasilishwa.
Mussa alisema zaidi ya tume tatu tayari zimeundwa, lakini ripoti hizo zimekaliwa na kufichwa ukweli kwa lengo la kuwafumbia macho waliohusika na ubadhirifu huo katika misingi ya kulindana.
“NLD inalitaka Baraza la Wawakilishi kukifuta kifungu cha Katiba ya Zanzibar cha 36(1) kisemacho hakuna mashitaka yoyote ya jinai yatakayofunguliwa au kuendelezwa dhidi ya Rais wakati akiwa kazini au dhidi ya mtu yeyote ambaye anafanya kazi ya urais kwa mujibu wa kifungu cha Katiba hii,” alisema Mussa akinukuu sehemu ya Katiba ya Zanzibar.
Kifungu hicho hutumiwa vibaya na Rais na kundi la wapambe wake, ili kuwalinda wanapokuwa madarakani na kufanya miradi ya kifisadi na kudidimiza uchumi wa nchi.
“Yapo majenereta 32 ya kuzalisha umeme ambayo ni mabovu, yamenunuliwa kwa fedha za SMZ, kuuzwa viwanja na majengo ya Serikali, fukwe na maeneo ya wazi, meli ya MV Mapinduzi imeuzwa kwa bei chee, wananchi wanyonge wakiporwa ardhi na vigogo wa Serikali hayo yameshuhudiwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Sita Zanzibar,” alisema.
CHANZO: GAZETI LA MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment