Home » » Ajira ngumu tishio jipya kwa ustawi wa watoto

Ajira ngumu tishio jipya kwa ustawi wa watoto

Watoto hawa ni miongoni mwa watoto wengi wanaofanya kazi za kugonga kokoto na kuchonga matofali kisiwani Pemba.  Watoto wengi wanatumikishwa katika ajira hiyo ngumu, huku wakikosa haki yao ya kupata elimu. Picha na Talib Ussi.  

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi kupitia mradi wa kupambana na ajira ngumu kwa watoto,  zaidi ya watoto 15,000 wanajishughulisha na ajira tena zile ngumu.
Wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikitimiza miaka 50 tangu Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyojenga mazingira mazuri ya maendeleo, visiwa vya Unguja na Pemba vimeathirika na ajira ngumu zinazowahusisha watoto.
Hicho ni kikwazo kinachoweza kuifanya Zanzibar ishindwe kuyafikia Malengo ya Milenia, ambayo yanataka hadi kufikia mwaka 2015 watoto wote wapate fursa na haki za msingi za elimu.
Vichocheo vya  ajira kwa watoto
Kwa Zanzibar sababu ni nyingi, ikiwamo wazazi kutokuwa na mwamko wa kuwasomesha watoto wao na kutamalaki kwa umaskini katika familia nyingi.
Hata hivyo,  wapo wazazi walioamua tu kuwatumikisha watoto wao katika ajira ngumu, huku wakisingizia kuwa wanafanya hivyo kwa sababu ya ugumu wa maisha.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi kupitia mradi wa kupambana na ajira ngumu kwa watoto, zaidi ya watoto 15,000 wanajishughulisha na ajira tena zile ngumu.
 Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) ambacho ni sehemu ya washiriki wa mradi, Sheha Haji Dau, anasema waliwatembelea watoto zaidi ya 264 na kubaini 80 wanaishi katika mazingira hatarishi kwa kujishughulisha na ajira ngumu.
Baada ya kuwabaini anasema wamekuwa wakihakikisha wanarudi shule kama anavyosema: “Kijiji cha Charawe pekee watoto 16 wamerudishwa shule. Wanaendelea vizuri na masomo, huku tukitoa elimu kwa wazazi wafuatilie maendeleo yao. ‘’
Hali mbaya Pemba
Kisiwa cha Pemba kinatajwa kuathirika zaidi kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi hata ndani ya familia zao.
Mratibu wa asasi ya kiraia inayoshughulikia mapambano ya ajira ngumu za watoto katika Mkoa wa Kaskazini Pemba  (Kukhawa), Mgeni Hamad Othman anasema ajira za watoto zimerudisha nyuma maendeleo ya sekta ya elimu katika kisiwa cha Pemba.

Chanzo;mwananchi

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa