SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeonya vyombo vya habari kwamba
haitosita kuvichukulia hatua za kisheria ikiwemo kuvifungia vyombo
vitakavyotumia vibaya uhuru wa vyombo vya habari kwa kuchapisha na kutoa
habari zenye lengo la kuvuruga amani.
Kauli
hiyo imetolewa jana na Waziri wa Habari Utangazaji Utalii na Michezo,
Said Ali Mbarouk, wakati alipokutana na viongozi na wahariri wa redio
binafsi ya Zenj FM pamoja na Coconut.
Redio
hizo hivi karibuni zilirusha moja kwa moja kongamano la wastaafu wa
vikosi vya ulinzi na usalama, ambapo azimio lao kuu lilikuwa utengano
kwa watu wa Pemba na Unguja. Akifafanua zaidi, Mbarouk alisema SMZ yenye
sura ya Umoja wa Kitaifa kwa sasa imetulia na malumbano ya kisiasa
yaliyokuwepo zamani yamemalizika na wananchi wanaishi vizuri kwa pamoja.
Alisema
chokochoko za aina hiyo pamoja na kauli hizo, kamwe hazitaachiwa
zichukuwe nafasi tena ya kuleta mgawanyiko wa wananchi ambao kwa sasa
wamemaliza tofauti zao tangu kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
'Sisi
tukiwa wasimamizi wa sera za Serikali hatutasita kuvichukuliya hatua
kali za kisheria vyombo vya habari vyenye lengo la kuwagawa wananchi kwa
kutumia kisingizio cha uhuru wa vyombo vya habari......uhuru wa vyombo
vya habari upo lakini una mipaka yake'alisema.
Aliwataka
viongozi na wahariri kuwa makini sana kuhakikisha waandishi waliopo
chini ya dhamana zao wanafuata maadili ya fani na taaluma ya uandishi wa
habari na kamwe kutoruhusu vyombo hivyo kutumika kinyume na maadili kwa
maslahi ya watu wachache.
Karipio
la Waziri Mbarouk limekuja ambapo hivi karibuni redio hizo zilirusha
moja kwa moja hewani makongamano yaliyotayarishwa na umoja wa askari
wastaafu yakiwa na matamshi mazito ya kuwataka wananchi wa visiwa viwili
hivi kutengana.
Katika
mikutano miwili iliyofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la
Wawakilishi hapo Kikwajuni na huko Makunduchi, wastaafu hao walionesha
kutofurahishwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliopo sasa
inavyoendeshwa chini ya Rais Dk Ali Mohamed Shein kusema imeshindwa
kuimarisha amani na utulivu kufuatia kujitokeza kwa matukio mbali mbali
ya watu kumwagiwa tindikali.
Aidha
Mbarouk ameitaka Tume ya Utangazaji kufuatilia vyombo vya habari na
kuona kwamba wanatekeleza na kufuata masharti waliyopewa ya leseni za
kurusha matangazo kwa wananchi.
Ofisa
Mwandamizi wa Redio ya Zenj FM Suleiman Juma Kimea alikiri kutokea kwa
kasoro mbalimbali katika baadhi ya vipindi vilivyorushwa hewani moja kwa
moja katika makongamano hayo na kusema kwamba hayatorudiwa tena.
“Tunakiri
kujitokeza kwa kasoro mbali mbali katika matangazo yaliyorushwa hewani
moja kwa moja na kituo chetu na tunaahidi kwamba hayatojitokeza tena,'
alisema.
Chanzo:Habari Leo
0 comments:
Post a Comment