Home » » Shein akerwa bidhaa zilizokwisha muda kuzagaa nchini

Shein akerwa bidhaa zilizokwisha muda kuzagaa nchini

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein
 
Rais  wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein ameitaka Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kuongeza jitihada katika kukabiliana na tatizo la bidhaa zilizokwisha muda hapa nchini.
Aidha, ameagiza kuwapo kwa uangalizi wa karibu na wa mara kwa mara na kuongeza umakini katika ukaguzi wa bidhaa zilizopo sokoni na wakati zinapoingizwa nchini.

Dk. Shein alitoa agizo hilo jana wakati akihitimisha kikao cha kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 na robo mwaka ya mwaka wa fedha 2013/2014, ikiwa ni mfululizo wa vikao hivyo vinavyofanyika Ikulu.

“Lazima sheria zizingatiwe katika kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopitwa na wakati haziendelei kuwapo katika soko la pamoja na kuangalia utaratibu wa kukagua ubora wa bidhaa kabla hazijashushwa bandarini ili kama hazikidhi masharti zisipewe fursa za kuingizwa nchini,” alisema.

Sambamba na agizo hilo, pia ameitaka wizara hiyo kuongeza juhudi za kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini hususan za wajasiriamali wadogo wakiwamo wakulima wa chumvi nchini.

Kuhusu uimarishaji na kuwajengea uwezo wajasiriamali nchini kupitia Programu ya Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), Dk. Shein aliitaka wizara kungalia namna bora ya kuhakikisha kuwa walengwa wa programu hiyo wanafikia malengo yaliyowekwa na hatimae kufaidika na programu hiyo.

Katika maelezo yake hayo Dk. Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, aliipongeza wizara hiyo kwa kutekeleza vyema malengo katika kipindi husika na kuongeza kuwa amevutiwa na mafanikio ya haraka ya Shirika la Biashara Zanzibar (ZSTC).
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

Post a Comment

 
Support by Blogs za Mikoa Tanzania
Copyright © 2012. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved
Designed by by Blogs za Miikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa